Membe:Chagueni mnayeona anafaa

20Oct 2020
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Membe:Chagueni mnayeona anafaa

MGOMBEA urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Bernard Membe, amesema wapiga kura wana uhuru wa kumchagua yeye au mgombea kwa tiketi ya Chama Cha Demokrasia na Mandeeo (CHADEMA), Tundu Lissu.

Membe ambaye alikuwa kimya kwa muda mrefu amesema ni lazima Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), zihakikishe uchaguzi unakuwa huru na haki kuepusha taifa kuingia katika vurugu.

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Membe ambaye hajaonekana katika majukwaa ya kampeni tangu arejee nchini kutokea Dubai mwanzoni mwa mwezi uliopita, alisema wapiga kura wako huru kuamua na kikubwa ni maendeleo ya watu.

Alisema Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe, na Mwenyekiti wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad, waliotangaza hadharani kumuunga mkono Tundu Lissu wanao uhuru wa kufanya hivyo na hilo kwake siyo tatizo.

“Wapo watu ndani ya CCM hawatampigia kura Magufuli, wapo watu ndani ya CHADEMA hawatampigia kura Tundu Lissu na wapo watu ndani ya ACT-Wazalendo hawatampigia kura Membe, ni haki yao wawili wameshasema, lakini wanaweza kubadili gia angani kura ni siri,” alisema Membe.

“Sisi ni wamoja, hatuna mgawanyiko wowote waliosema ni ‘individuals’ (binafsi) na tumeyamaliza Chama cha ACT-Wazalendo kina mgombea anaitwa Bernard Membe chama kile kama vyama vingine kimeorodheshwa kwenye fomu ya wagombea urais 15 nipo namba 9 pale,” aliongeza Membe.

Vile vile, aliitaka NEC kutenda haki kwa kutangaza matokeo halali ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, ili kuepusha kile alichokiita fujo baada ya uchaguzi.

Kwa mujibu wa Membe, utafiti alioufanya yeye na wenzake kuna dalili za kutokea matatizo katika nchi na kusema kuwa dawa pekee ni kutenda haki.

“Moja kati ya haki inayotakiwa ni ile ya kukubali matokeo na kumtangaza mshindi hata kama wewe umeshindwa na unajiona una pembe sita kubali matokeo,” alisema.

Katika suala la kuepusha vurugu, Membe amewataka viongozi wa dini ambao baadhi yao tayari wamejitokeza hadharani kuwaunga mkono baadhi ya wagombea, kuacha mara moja kufanya hivyo, ili kuepusha nchi kuingia katika mgogoro wa kidini jambo ambalo amesema ni la hatari iwapo litaendelea.

Kuhusu upigaji kura ya mapema Zanzibar, alishauri iondolewe na ibakize siku moja pekee ya kufanyika uchaguzi, tofauti na ilivyo sasa kwa kuwekwa siku mbili za kupiga kura ambazo ni Oktoba 27 na Oktoba 28.

Alisema kwa uzoefu wake katika kusimamia uchaguzi barani Afrika katika nchi 19 kama mwangalizi wa uchaguzi, kura mbili liliwahi kujitokeza katika baadhi ya nchi na lilileta matatizo.

“Suala la kupiga kura siku mbili linajenga hisia ya tatizo kutokea mimi kama mwanasiasa mbobevu niliyekwenda nchi 19 kusimamia uchaguzi hili linaweza kuwa tatizo kubwa,” alisisitiza Membe.

Alipoulizwa juu ya yeye kutokufanya kampeni, alisema chama hicho bado kichanga na hakina uwezo wa kifedha na kwamba wameelekeza nguvu kwa wagombea udiwani na ubunge katika maeneo 100 nchini.

Akizungumzia sera za chama hicho iwapo kitachaguliwa kuingia madarakani Membe, alisema serikali yake itaweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara ili wawe huru na kuahidi kuwashushia kodi ili waweze kupata faida jambo ambalo amedai halifanyiki kwa sasa na hivyo kufanya wafanyabiashara hao kuwa na mazingira magumu.

Kuhusu kilimo alisema akiwa rais bei ya mazao ya wakulima kama kahawa, pamba, mbaazi na korosho  itaamuliwa na soko huku serikali ikipewa kodi pekee na kwamba serikali yake kamwe haitaingilia bei za mazao ya wakulima.

Kuhusu ajira, alisema serikali yake itatumia fedha ili sekta binafsi ziweze kunufaika na fedha hizo na hivyo kukua jambo ambalo litawezesha sekta hizo kuwa na uwezo wa kuajiri na kupunguza tatizo la ajira nchini.

Kwa upande wa uhusiano wa kimataifa, Membe alisema serikali yake itaimarisha uhusiano wa kimataifa ili kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya nchi.

*Imeandikwa na Enock Charles na Frank Maxmillian (TUDARCo).

Habari Kubwa