Meneja adaiwa kutakatisha mil. 413/-

23Oct 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Meneja adaiwa kutakatisha mil. 413/-

MENEJA wa Kampuni ya Neelkani Salt Limited, Mohammed Alikhan (29), amefikishwa mahakamani akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi ikiwamo wizi wa katoni za chumvi 45,919 zenye thamani ya Sh. milioni 413.5.

Alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Janeth Mtega, aliyepangiwa kusikiliza kesi yake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, alidai kuwa kati ya Januari Mosi, 2018 na Julai 29, mwaka huu mshtakiwa anadaiwa kutenda makosa hayo.

Wankyo alidai kuwa kati ya Januari Mosi, 2018 na Julai 29, mwaka huu katika mtaa wa Arusha Ilala, jijini Dar es Salaam, Alikhan akiwa Meneja wa tawi la kampuni hiyo aliiba katoni za chumvi 45,871 aina ya Neel, mali ya mwajiri wake yenye thamani ya Sh. 412,839,000.

Katika shtaka jingine, mshtakiwa huyo anadaiwa kuwa katika kipindi hicho aliiba kilo moja ya aina ya Neel Gold yenye thamani ya Sh. 720,000.

Jamhuri ilidai katika tarehe na miaka ya tukio la kwanza, mshtakiwa Alikhan alitakatisha Sh. 413,559,000, wakati akijiua fedha hizo zimetokana na zao la makosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na wizi akiwa mwajiriwa.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa sababu mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo mpaka upelelezi utakapokamilika na itahamishiwa Mahakama Kuu Divisheni ya Uhujumu na Rushwa.

Hakimu alisema kwa kuwa mashtaka ya kutakatisha fedha hayana dhamana, mshtakiwa atarudishwa mahabusu.
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na mshtakiwa alipelekwa rumande. Kesi imeahirishwa hadi Novemba 5, mwaka huu.

Habari Kubwa