Meneja Finca, wenzake kortini tuhuma za wizi

30Nov 2020
Joctan Ngelly
Geita
Nipashe
Meneja Finca, wenzake kortini tuhuma za wizi

WAFANYAKAZI wanne wa Benki ya Finca Tawi la Geita, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita kwa makosa mawili ya wizi wa Sh. milioni 33.

Wanadaiwa kuwa wakiwa na nia ya kudanganya, waliwasilisha ripoti za uongo za kimahesabu, ambapo ripoti yao ilionyesha kwamba salio lililokuwapo kwenye benki yao katika mahesabu ilikuwa Sh. 76,880,300 wakati uhalali ni Sh. 47,880,300 kinyume cha kifungu cha 317 (b) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2019.

Washtakiwa hao waliofikishwa mahakamani ni Maria Mwakapala (32) wa kitengo cha mapokezi benki ya Finca, Philip Dahaye (35), mhasibu, Francis Kazaura (39), Meneja na Furaha Twinzi (21) ambaye ni mlipaji mkuu wa benki hiyo.

Washtakiwa wote kwa pamoja walipandishwa kizimbani Ijumaa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Obadia Bwegoge na waliwasomea mashtaka yao mawili, lakini waliyakana.

Washtakiwa wako nje kwa dhamana ya wadhamini wawili wawili, ambao walitoa barua za utambulisho kutoka kwa ofisa mtendaji wa kata na mali isiyohamishika yenye thamani ya Sh. milioni 4 kwa kila mdhamini.

Upande wa mashtaka ukiongozwa na Wakili wa Serikali, Masambu Danieli, ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo namba 376/2020 umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali.

Hakimu Bwegoge alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Desemba 10, mwaka huu kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa hao maelezo ya awali.

Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali Masambu Danieli alidai kwa tarehe tofauti na muda kati ya Januari na Mei mwaka huu, katika Benki ya Finca Tawi la Geita katika Wilaya na Mkoa wa Geita, washtakiwa wakiwa waajiriwa wa Benki ya Finca, waliiba kiasi cha Sh. milioni 33 mali ya benki hiyo.

Danieli aliendelea kudai kuwa kosa la pili washtakiwa wote kwa pamoja wakiwa na nia ya kudanganya, waliwasilisha ripoti za uongo za kimahesabu, ambapo ripoti yao ilionyesha kwamba salio lililokuwamo kwenye benki yao katika mahesabu ilikuwa ni Sh. 76,880,300 wakati uhalali ni Sh. 47,880,300 kinyume cha sheria.

Habari Kubwa