Mengi asimulia alivyoagana na Mkurugenzi Mipango IPP

20Mar 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Mengi asimulia alivyoagana na Mkurugenzi Mipango IPP

MWENYEKITI Mtendaji wa  IPP, Dk. Reginald Mengi, amesimulia alivyoagana na aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango wa IPP, Francis Zangira, aliyefariki Machi 9, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Mwenyekiti Mtendaji wa IPP na mkewe Jacqueline Mengi, wakitoa heshima za mwisho mbele ya mwili wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango wa IPP, Francis Zangira, nyumbani kwa marehemu Mbezi Tangi Bovu, Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: SELEMANI MPOCHI

Katika ibada ya kuaga mwili wa Zangira iliyofanyika nyumbani kwake, Mbezi Tangi Bovu, jijini Dar es Salaam, Dk. Mengi alisema alikuwa sehemu ya maisha yake.

“Mengi yamezungumzwa juu ya Francis na mimi niseme machache kwa sababu alikuwa sehemu ya maisha yangu. Juu ya tabia yake nilishuhudia kwa vitendo. Niwape mfano mmoja, siku moja gari lake lilikuwa limeharibika, nikamwambia kwa nini asikodi gari, akakataa akasema ni gharama sana,” alisema Dk. Mengi na kuongeza:

“Francis tulikutana naye mara ya mwisho kabla ya kufariki dunia. Alikuja ofisini kwangu kuniambia kwamba anaomba kupumzika na nikamwambia utaondokaje IPP wakati wewe ni sehemu yake? Lakini yeye alisema amechoka sana anaomba kupumzika. Nilimwambia kwamba hawezi kustaafu hivi hivi kwa sababu alikuwa sehemu ya IPP na ina jasho lake.

“Basi mwanasheria akanipatia barua yake na mimi nikaiidhinisha na nikamwambia unaondoka lakini huwezi kuondoka hivi hivi. Naomba uondoke na ukapumzike lakini upatiwe mshahara na marupurupu yako yote.”

Dk. Mengi alisema baadhi ya vitu ambavyo alimwahidi Zangira kabla ya kufariki dunia ni pamoja na kumpatia usafiri, nyumba na hivyo alitoa maelekezo kuhakikisha mjane anapatiwa vyote pamoja na mshahara aliokuwa akipata mumewe kila mwezi katika maisha yake yote.
“Francis ametuacha wapweke na Mungu atamsaidia huko anakokwenda,” alisema Dk. Mengi.

Akisoma wasifu wa baba yake, mtoto wa marehemu, Lulu, alisema Zangira alikuwa tegemeo na msaada kwa watoto na familia nzima kwa ushauri na alijitahidi kuweka furaha.

“Nashukuru kwamba Mungu alinipa kibali. Tulikuwa naye siku zake za mwisho, nilikuwa naongea naye kila siku na nilikuwa nakutana naye kila wiki. Asiponipata au kumpata mtoto wake yeyote alikuwa anajitahidi kuhakikisha anampata. Alikuwa na ubinadamu, msheshi, mwenye busara, mtu wa watu na mwadilifu,” alisema.

“Hakuwa mtu ambaye alikuwa anajitahidi afahamike kwa alicho nacho. Alijulikana kwa kuweka furaha kwa sura za watu. Tumepoteza si tu baba bali rafiki na yeyote niliyeongea naye alisema hicho kiatu atavaa nani. Alikuwa kiungo katika familia, si kwa mali bali kwa busara, hata kwa marafiki zangu alikuwa kama baba yao,” aliongeza Lulu.

“Kuna kaka mmoja anauza magazeti alikuwa ananisimulia kwamba siku ya mechi ya Simba dhidi ya AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC) angempitia waende kuangalia mechi, hivi ndivyo alivyokuwa baba yetu.”

Mmoja wa Wakurugenzi wa IPP, Joyce Luhanga, alisema Zangira alikuwa mtu aliyekuwa na taaluma ya uchumi kama yeye kwa hiyo muda mwingi walikuwa wanashauriana mambo mengi na kwamba alifanya naye kazi kwa miaka 25.

“Alikuwa mtu wa karibu na kwa sababu alikuwa mchumi kama mimi. Siku za mwanzo tulikuwa tunafanya kazi zinazofanana na kila siku ya Mungu tulikuwa tunaonana ama kusalimiana au ‘ku-consalt’  kuhusu jambo fulani. Kwa hiyo tulikuwa ‘tuna-share’ vitu vingi na nashukuru Mungu kwamba alinipa nafasi ya kuwa na mtu wa karibu mwenye busara sana,” alisema Luhanga.

Aliongeza kuwa: “Nimejifunza mengi kutoka kwake na nina uhakika watu wengi tulio nao ofisini wamejifunza mengi kutoka kwake.

Alikuwa anaishi maisha ya kawaida sana. Mara nyingi alikuwa anapita na usimjue kama ni bosi pale ofisini na ilikuwa rahisi kumchanganya kama mtu wa kawaida, lakini ‘that is humble he was’ na alikuwa anajiweka nyuma wakati wote labda mpaka utambue kwamba yeye ni bosi.”

“Kwa hiyo tumempoteza rafiki wa karibu sana na tutamkumbuka siku zote. Daima alikuwa mtu wa kucheka na kila mtu na najua marafiki zake wengi pale ofisini itawachukua muda mrefu kusahau kwa sababu alikuwa akiingia unatambua kwamba ameingia.”

Alisema Zangira baada ya kuanza kuugua, aliwaambia kuhusu hali ya afya yake na aliomba kupumzika.

“Alivyoanza kuugua alikuwa ‘ana-share’ kuhusu hali ya afya yake na akasema kwamba ameamua atapumzika kazi kwa sababu anaona afya yake inadorora. Tukashirikishana kwa hilo na kweli akaruhusiwa kupumzika na kabla haya hayajatimia ndiyo Mungu akamtwaa. Ni masikitiko makubwa kwetu familia ya IPP, tutamkumbuka na kumwombea siku zote,” alisema Luhanga.

Habari Kubwa