Meya ampongeza JPM kuondoa hofu corona

06Aug 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Meya ampongeza JPM kuondoa hofu corona

KAIMU Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Abdalah Mtinika, amempongeza Rais John Magufuli kwa mikakati imara ya kukabiliana na tishio la corona na kuwapa ujasiri wananchi kutokuwa na hofu ya virusi hivyo.

Mtinika alitoa pongezi hizo jana jijini Dar es Salaam wakati alipozungumza katika hafla ya uzinduzi wa kampeni iliyoandaliwa na WaterAid inayolenga kupambana na magonjwa ambukizi ambayo chanzo chake ni uchafu unaotokana na kutokunawa kwa majisafi na sabuni.

Meya huyo alisema kunawa mikono kutaepusha siyo tu kupata virusi vya corona, bali pia magonjwa zaidi ya saba ambayo silaha ya kuyaangamiza ni usafi wa mwili hasa kunawa mikono mara kwa mara kwa maji yanayotiririka.

"Unaponawa mikono mara kwa mara kwa maji yanayotiririka, unaepukana na magonjwa mengi yanayoambukizwa kama vile corona, kipindupindu, kichocho na magonjwa mengine ambayo chanzo chake ni kutokunawa mikono na sabuni," alisema.

Meya huyo pia aliishauri taasisi hiyo kufika mbali zaidi kuifikisha elimu hiyo kwa jamii hususani mitaani na kwa wanafunzi wa shule mbalimbali nchini ili elimu ienee zaidi nchini.

"Ninawashauri WaterAid kwamba uzinduzi wa kampeni hii ya 'Usichukulie Poa Unategemewa', ihusishe na utoaji wa elimu kuanzia mitaani pamoja na shuleni ambako ndiko kuna kizazi cha baadae na hilo litasaidia sana katika kuhakikisha tunafika mbali na kampeni hiyo.

"Hatuwezi kuifikisha elimu kote kwa kutumia waandishi wa habari tu, ila utoaji wa elimu mtaa kwa mtaa ni muhimu zaidi," kiongozi huyo alisisitiza.

Mkurugenzi Mkazi Mradi wa WaterAid, Anna Mzinga, alisema wataendelea kuiunga mkono serikali katika kukabiliana na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya uchafu unaotokana na watu kutokuwa na utamaduni wa kunawa kwa maji tiririkia na sabuni.

Alisema kampeni hiyo iliyozinduliwa jana imewashirikisha wasanii mbalimbali na mchezaji wa mpira wa miguu, Juma Kaseja watakaotoa elimu kwa jamii katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Geita na Zanzibar.

"Kampeni hii itaendelea hadi Januari na itahusisha kusambaza na kueneza ujumbe wa mabadiliko ya tabia ya usafi kupitia vyombo vya habari pamoja na matukio ya ushiriki wa jamii," alisema Mzinga.

"Magonjwa haya ni mengi sana na serikali inajitahidi kupambana na magonjwa ambukizi kwa lengo la kufanya kila mtu awe na afya imara, aweze kuendelea na shughuli za kulijenga taifa letu, hivyo tupo nao bega kwa bega kwa kuwa sisi ni wadau wa maji," aliongeza.

Balozi katika kampeni hiyo, Mrisho Mpoto, alisema ni aibu kubwa kuona mtu anapata maradhi kutokana na uchafu na kutokunawa mikono kwa majisafi na sabuni.

Habari Kubwa