Meya Dar asota 'selo' siku mbili

03Dec 2018
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Meya Dar asota 'selo' siku mbili

MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita, anashikiliwa na Jeshi la Polisi katika Kituo cha Chang'ombe kwa tuhuma za kufanya maandamano bila kuwa na kibali.

MEYA wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita

Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alithibitisha kukamatwa na kushikiliwa kwa meya huyo, akibainisha kuwa alikamatwa juzi jioni Vijibweni ambako ni kwenye kata yake.

Alidai meya huyo alikutwa katika eneo hilo akiongoza maandamano kuelekea Daraja la Mwalimu Nyerere, hivyo wanamshikilia kwa kosa la kuongoza maandamano yasiyo halali.

"Bado tunamshikilia, tulitaka kumhoji ili tumwachie kwa dhamana, lakini alikataa kwa madai kuwa hawezi kuhojiwa hadi mwanasheria wake afike, nasi tulimwacha aendelee kukaa ndani hadi mtu wake atakapofika," alisema Mambosasa.

Hata hivyo, baadhi ya watu wa karibu na meya huyo ambaye pia ni Diwani wa Vijibweni, waliiambia Nipashe jana, kuwa wakati anakamatwa na polisi, alikuwa kwenye ziara ya kichama ya kufungua tawi la vijana wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alisema Mwita juzi, alikuwa kwenye kata yake akifanya kikao cha Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha).

Alisema kuwa alipomaliza kikao majira ya jioni, alifuatana na vijana aliokuwa nao kwenye mkutano kwenda kufungua tawi la vijana karibu na eneo la mkutano.

"Wakati wakiwa njiani kuelekea huko, walitokea polisi waliwatawanya vijana kwa mabomu na kisha kumkamata meya na kumpeleka Kituo cha Polisi Chang'ombe, Mkoa wa Kipolisi Temeke, ambako anashikiliwa hadi sasa," alisema Mrema.

"Mawakili wetu wanapambana ili atolewe. Tunalaani watu kukamatwa wakiwa kwenye vikao vya ndani na hawajavunja sheria yoyote na tunalitaka Jeshi la Polisi lifanye kazi kwa kufuata misingi ya kanuni, taratibu na sheria kuliko mihemko." 

Habari Kubwa