Meya Ubungo atangaza kung’atuka udiwani

07Apr 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Meya Ubungo atangaza kung’atuka udiwani

MEYA wa Manispaa ya Ubungo jijini Dar es salaa, Boniface Jacob, amesema hatogombea tena nafasi ya udiwani katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka huu, na kuweka wazi nia yake ya kugombea ubunge endapo chama chake kitaridhia.

MEYA wa Manispaa ya Ubungo jijini Dar es salaa, Boniface Jacob, picha mtandao

Katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter, Jacob alitangaza kutokugombea nafasi ya udiwani na alipoulizwa kama ana mpango wa kugombea ubunge, alijibu atakuwa tayari kufanya hivyo kama chama chake kitaridhia.

Katika ukurasa wake huo, Jacob alisema kwa kipindi cha miaka 10 alichotumikia katika nafasi yake hiyo ya udiwani imetosha.

“Nimetangaza kung’atuka katika udiwani Kata ya Ubungo muda wa madiwani utakapoisha, sitogombea tena udiwani uchaguzi ujao,”aliandika ujumbe huo Jacob katika ukurasa wake huo.

Aliongeza: “Miaka 10 ya utumishi wangu ni kwa sababu Wana-Ubungo mlinikopesha imani, tumekuwa wote wakati wa shida na raha, mabonde na milima.”

Jacob ametangaza msimamo wake huo wa kutokugombea nafasi ya udiwani huku kukiwa na tetesi zinazodai kwamba mpango wake ni kusogea katika hatua nyingine ya kugombea ubunge.

Hivi karibuni, wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), walikwenda nyumbani kwa Meya huyo na kumuomba agombee nafasi ya ubunge katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Wananchi waliokwenda nyumbani kwa Meya huyo kumuomba agombe nafasi hiyo ya ubunge ni wa wale wanaoishi Ubungo ambao pia walidhihirisha nia yao hiyo kwa kusaini katika karatasi waliyokuwa wamejiorodhesha.

Akizungumza na Nipashe, Jacob alisema yuko tayari kutumikia nafasi nyingine ya juu kisiasa endapo atapewa ridhaa na chama chake.

“Kwa kweli kwa kipindi hiki ambacho nimetumia katika nafasi ya udiwani kimenitosha, nimefanya mambo mengi ambayo naamini hata wananchi wameridhika, sasa nimekomaa, niko tayari kusonga mbele kidogo ili nipambane na changamoto nyingine kubwa zaidi,” alisema Jacob.

Aliongeza: “Mimi ni kama kiraka, niko tayari kugombea nafasi ya Ubunge katika jimbo lolote ambalo viongozi wangu wataridhia.”