Mfanyabiashara abambwa na doti 600 za CCM

04Jul 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Mfanyabiashara abambwa na doti 600 za CCM

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Shinyanga, imemkamata mfanyabiashara wa magari ya teksi, Joseph Tasia, akiwa na doti 600 za vitenge vyenye nembo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) nyumbani kwake na kushindwa kutoa maelezo yanayojitosheleza.

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), mkoani Shinyanga, Hussein Mussa, akionyesha doti 600 za vitenge vyenye nembo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambavyo vimekamatwa kutoka kwa mfanyabiashara wa usafiri wa magari madogo (TAXI), Johas Tasia, vikiwa nyumbani kwake, eneo la Mwasele, mjini Shinyanga, kwa ajili ya kushawishi wapiga kura ndani ya chama hicho. PICHA: MARCO MADUHU

Mkuu wa Takukuru mkoani humo, Hussein Mussa, katika taarifa yake jana alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa Juni 29, saa 3:00 usiku mtaa wa Mwasele B.

Mussa alisema walimkamata Tasia akiwa na doti hizo zikiwa zimehifadhiwa nyumbani kwake jambo ambalo linaashiria kuwa zilikuwa zinaandaliwa kutumika katika kufanya ushawishi kwa wapigakura.

"Uchunguzi wa Takukuru mkoani Shinyanga umebaini Tasia mfanyabiashara wa magari madogo ya teksi hana duka wala hafanyi biashara ya kuuza vitenge," alisema.

Aidha, alisema katika mahojiano alishindwa kutoa maelezo yanayotosheleza kuhusiana na mzigo huo aliokutwa nao na hata nyaraka za ununuzi alizowasilisha hazijitoshelezi, hivyo kuonyesha shaka juu ya uhalali wake.

"Uchunguzi wa kina wa tukio hili unaendelea ili kubaini iwapo vilikuwa kwa ajili ya kuhusiana na vitendo vya rushwa katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba, mwaka huu au ni kwa ajili ya kufanya biashara katika msimu huu," alisema.

Mussa alisema ofisi hiyo inawaonya watu wote wenye nia ya kutumia taarifa zozote za uchunguzi zinazofanywa nao kwa nia ya kujinufaisha kisiasa kwani kitendo hicho ni kuingilia uchunguzi na ni kosa la jinai na atakayebainika atachukuliwa hatua," alisisitiza.

Habari Kubwa