Mfanyabiashara ajimiminia risasi na kufariki

30Mar 2020
Gideon Mwakanosya
Songea
Nipashe
Mfanyabiashara ajimiminia risasi na kufariki

MFANYABIASHARA na mkandarasi, mkazi wa Mpambalyoto, Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Justin Rwendera (64), amekutwa amekufa baada ya kujifyatulia risasi mdomoni na kutokea kwenye sikio la mkono wa kulia.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, picha mtandao

Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa, alisema tukio hilo lilitokea Machi 29, saa moja asubuhi nyumbani kwake mtaa wa Mpambalyoto.

Alisema kuwa inadaiwa siku ya tukio majira ya saa moja asubuhi, Amida Mnali (47), mkazi wa Bombambili, Songea Mjini, mpishi wa Rwendera na mfanya usafi kwenye nyumba hiyo, aliingia ndani na kumkuta bosi wake akiwa amelala kwenye kochi huku chini kukiwa na bunduki aina ya pisto na damu nyingi zikiwa zimetapakaa. Alisema aliamua kutoa taarifa kwa kuwajulisha ndugu na polisi kuhusu tukio hilo.

Alisema kuwa Machi 28, majira ya saa 11 jioni, Rwendera alirudi nyumbani kwake kutoka kwenye matembezi akiwa amelewa na kukuta kijana wa kaka yake Raurian Bathromeo (43), ambaye ni dereva wa greda linalomilikiwa na marehemu na kumwomba ampatie chakula.

Alisema baada ya kula chakula hicho muda mfupi alitoka kuelekea kwenye zizi la ng’ombe kisha mtoto wa kaka yake aliondoka kwenda nyumbani kwake eneo la Ruvuma.

Kamanda Maigwa alisema polisi walipofika katika eneo la tukio, walikuta bastola ikiwa na risasi saba pamoja na ganda moja la risasi huku mwili wake ukiwa kwenye kochi.

Alisema kuwa bunduki hiyo inashikiliwa na Jeshi la Polisi wakati uchunguzi wa tukio hilo ukiwa unaendelea na hakuna mtu yeyote anayeshikiliwa kuhusiana na tukio hilo, chanzo cha tukio hakijajulikana na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea.

Habari Kubwa