Mfanyabiashara aliyetishia kuua atiwa hatiani kortini

04Dec 2022
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Mfanyabiashara aliyetishia kuua atiwa hatiani kortini

MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala imemtia hatiani Mfanyabiashara wa Kariakoo, Adelard Lyakurwa kwa kosa la kutishia kumuua kwa bastola mfanyabiashara mwenzake, Valence Lekule.

Hukumu hiyo ilisomwa jana mbele ya Hakimu Mkazi, Fadhili Luvinga kwa niaba ya Hakimu Mkazi, Glory Mkwera ambaye yuko kwenye kazi maalum.

Hakimu Luvinga alisema mshtakiwa anakabiliwa na shtaka moja la kutishia kuua kwa bastola, ikidaiwa kuwa Julai 30, 2020. maeneo ya Kariakoo, kwa nia ya kutaka kuua alimtishia kwa bastola Valence Lekule.

Alisema katika kesi hiyo upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi wanne na upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi watatu.

"Baada ya kupitia ushahidi wa pande zote mbili, mahakama imeona upande wa Jamhuri umethibitisha mashtaka bila kuacha shaka, hakuna shaka kwamba kulikuwa na tishio la kutumia bastola.

"Mahakama imeona mashahidi wa Jamhuri wa kuaminika na ushahidi wa upande wa utetezi hauna mashiko.

"Mahakama imeridhika kwamba upande wa Jamhuri umethibitisha kosa dhidi ya mshtakiwa, hivyo mahakama inamtia hatiani," alisema Hakimu Luvinga.

Akiomba mahakama impunguzie adhabu mteja wake, Wakili Richard Mbuli alisema ni mkosaji wa mara ya kwanza, anasumbuliwa na maradhi ya  vidonda vya tumbo na presha na familia inamtegema, hivyo aliomba apewe adhabu ndogo.

Akitoa adhabu, Hakimu Luvinga alisema mahakama imezingatia hoja zilizowasilishwa, inampa adhabu ya kifungo cha miezi 12 jela au faini ya Sh. milioni moja.

Pia alisema mahakama inaamuru kielelezo cha silaha na kitabu chake vitaifishwe, vitakabidhiwa kwa mamlaka inayohusika. Mshtakiwa alifanikiwa kulipa faini na akaachiwa huru.

Hata hivyo, akizungumza baada ya hukumu hiyo, Lekule alidai hakuridhishwa na uamuzi wa mahakama na anatarajia kukata rufani.

Habari Kubwa