Mfanyabiashara kizimbani kwa kutakatisha bil. 188.9 kwa EFD

07Dec 2018
Hellen Mwango
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mfanyabiashara kizimbani kwa kutakatisha bil. 188.9 kwa EFD

MFANYABIASHARA  Mustapha Kambangwa (34)  amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, akikabiliwa na tuhuma za Uhujumu Uchumi ikiwamo kutakatisha Sh. bilioni 188.9 kwa kupitia mashine ya kilekroniki ya EFD.

MFANYABIASHARA  Mustapha Kambangwa (34) .

Kambangwa alisomewa mashtaka yake mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtenga.

Wakili wa Serikali Mwandamizi,  Christopher Msigwa alidai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na mashitaka manne kati ya Juni Mosi ,2016 na Novemba 2, mwaka huu alitenda makosa hayo.

Katika shtaka la kwanza, Kambangwa alijifanya kama mtu aliyesajiliwa kuwa mlipa kodi ya ongezeko la thamani (VAT), kati ya Juni Mosi, 2016 na Novemba 2, mwaka huu  jijini Dar es Salaam, alikusanya   Sh. 188,928,752,166 kwamba anakusanya fedha hizo kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la pili, ilifaiwa kuwa kati ya Juni Mosi, 2016 na Novemba 2, mwaka huu, Kambangwa kwa udanganyifu alitumia mashine ya kieletroniki ya EFD yenye namba 03TZ842011315 iliyosajiliwa kwa jina la Kampuni ya Abraham's Group LTD kukwepa kodi ya VAT yenye thamani ya fedha hiyo.

Upande huo wa Jamhuri ulidai  tarehe na kipindi hicho, mahali tofauti jijini Dar es Salaam alitakatisha, alijipatia au kujimilikisha fedha hizo alizozipata kutokana na makato ya kodi ya VAT ambazo zilipaswa kutolewa kwa Kamishna wa TRA na mshtakiwa huyo alipaswa kujua kuwa fedha hizo ni zao la kosa la ukwepaji kodi.

Msigwa alidai katika tarehe tofauti kati ya Juni Mosi,2016 na Novemba 2,  mwaka huu jijini Dar es Salaam kwa  makusudi akiwa na nia  y kukwepa kodi alitumia mashine ya kieletroniki  ya EFD huku akijua kwamba hajasajiliwa kama mlipakodi ya VAT aliisababishia TRA hasara ya Sh.188,928,752,166.