Mfanyakazi benki mbaroni Shambulio Jenerali JWTZ 

14Sep 2017
Beatrice Shayo
Nipashe
Mfanyakazi benki mbaroni Shambulio Jenerali JWTZ 

JESHI la Polisi linamshikilia askari wa Suma JKT, Godfrey Gasper na mfanyakazi wa benki ya NBC kutokana na tukio la kujeruhiwa kwa Meja Jenerali mstaafu wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), Vincent Mritaba.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa.

Juzi, Meja Jenerali Mribata, akiwa anatoka benki ya NBC Tawi la Mbezi Beach eneo la Tangi Bovu, jijini Dar es Salaam, alivamiwa na watu wasiojulikana na kumjeruhi kwa risasi tumboni, mikononi na kiunoni alipofika nyumbani kwake, Tegeta Masaiti.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini jana, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, alisema jeshi hilo linawashikilia watu hao huku akieleza kuwa nyumba ya Jenerali Mritaba imekuwa ikilindwa na walinzi wa Suma JKT.

Alisema baada ya kufika nyumbani kwake vizuri, kama walivyoelezwa na mlinzi ambaye aliwajulisha kuwa huwa analinda mchana akiwa na silaha ya shortgun yenye namba za usajili TZCAR 96444.

“Alituambia mchana huwa analinda peke yake, lakini katika mazingira ya kushangaza aliiweka silaha juu ya kitanda kwenye kibanda cha mlinzi na kwenda kutoa ushirikiano kwa wahalifu kwa kwenda mikono mitupu kufungua mlango, wahalifu wakaingia kutenda uhalifu uliofanyika,” alisema Mambosasa.

”Baadaye anaeleza kuwa aliamuriwa kukimbia na yeye akakimbia na kuacha silaha halafu baadaye akairudia silaha hiyo."

Kamanda Mambosasa alisema askari huyo ambaye wana uhakika alipitia mafunzo ya JKT, mwenye dhamana ya kuhakikisha usalama wa maeneo wanayolinda, asingeenda kufungua geti bila kuwa na silaha.

Alisema mlinzi huyu alipewa silaha kwa ajili ya kulinda, hivyo kuna shaka ya msingi ya kuacha silaha na kutopigwa hata kofi na wahalifu hao.

“Wakati Meja Jenerali akishambuliwa, aliambiwa ondoka polepole na kutii bila hata kusindikizwa na kipigo chochote,” alisema Mambosasa.

Alisema walikwenda eneo la tukio na kubaini kuna mtu alikuwa anafanya mawasiliano kati ya mtoa huduma mmoja wa benki ya NBC na mtu mwingine aliyefanya mpango wa tukio hilo ambaye wanamshikilia kwa ajili ya mahojiano.

UVAMIZI OFISI YA MAWAKILI
Katika hatua nyingine, Kamanda Mambosasa alisema kuvamiwa kwa ofisi ya mawakili ya kampuni ya Prime Attorneys iliyoko jengo la Prime House, Tambaza, jijini Dar es Salaam, kunaendelea kuchunguzwa na makachero wake, ili kuwabaini waliohusika.

“Mpaka sasa bado hatujamkamata mtu yeyote kutokana na tukio la kuvunjwa kwa ofisi ya mawakili hao, lakini makachero wetu wanaendelea na uchunguzi wao,” alisema Kamanda Mambosasa.

Kamanda Mambosasa pia alitangaza kupiga marufuku uuzwaji wa silaha za jadi holela kama visu, mapanga na mishale na yeyote ambaye atakutwa akiuza atachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.

Habari Kubwa