Mfugaji mbaroni vifo simba Ruaha

17Feb 2018
Romana Mallya
Nipashe
Mfugaji mbaroni vifo simba Ruaha

SERIKALI inamshikilia mfugaji mmoja kwa uchunguzi baada kudaiwa kuhusika kuweka sumu kwenye mzoga na kusababisha vifo vya simba sita katika eneo la Usimamizi wa Wanyamapori (WMA) nje ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

BAADHI YA VIONGOZI NA WAHIFADHI WAKISHANGAA BAADA YA KUKUTA MIZOGA YA SIMBA SITA WANAODAIWA KUUAWA KWA KUTEGWA KWA SUMU.

Hatua hiyo imechukukuliwa baada ya taarifa iliyozagaa kwenye mitandao ya kijamii ikionyesha picha ya namna simba hao walivyokufa na mazingira yaliyosababisha  vifo hivyo.

Akizungumza na Nipashe jana, Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali Gaudance Milanzi, alisema tukio hilo linaonyesha kuwa mfugaji huyo aliamua kufanya ukatili huo baada ya mifugo yake kushambuliwa na wanyama hao.

Alisema mtu huyo aliweka sumu kwenye mzoga wa mifugo ambao simba hao walipoula walikufa.

“Serikali imeanza kulifanyia kazi suala hili ili kupata ufumbuzi. Tayari mtuhumiwa aliyedaiwa kufanya hivyo amekamatwa kwa mahojiano na sampuli zimepelekewa kwa mkemia mkuu wa serikali ili kujua ni aina gani ya sumu iliyotumika,” alisema.

“Vitendo vya namna hivi vinaweza kuleta madhara makubwa kwa maisha ya wanyama wengine pia vinaweza kuathiri binadamu,” alisema.

Alisema serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha matatizo kama hayo hayatokei tena siku za usoni ikiwamo kuepuka mwingiliano wa watu kwenye hifadhi.

“Napenda kuwaasa wafugaji na watu wenye tabia ya kuwapa sumu wanyama kwamba hatua hiyo inahatarisha uhai wa viumbe vingine ambavyo huwa vinakutwa vimekufa au vikiwa katika hali mbaya baada ya kula sumu ambayo huwekwa na watu kama alivyofanya mfugaji huyo,” alisema Jenerali Milanzi.

Juzi, mmoja wa wasimamizi wa Hifadhi ya Ruaha, alituma picha zinazoonyesha simba hao sita waliouawa kwa kupewa sumu katika eneo la usimamizi wa wanyamapori (WMA) nje ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

 

 

Habari Kubwa