Mfuko asasi zinazosaidia watu wenye ulemavu waja

18Mar 2019
Elizaberth Zaya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mfuko asasi zinazosaidia watu wenye ulemavu waja

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amesema serikali iko katika hatua za mwisho kukamilisha uanzishwaji mfuko wa kusaidia asasi zinazohudumia watu wenye ulemavu.

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akionyesha vitabu vya I can, I must, I will kilichoandikwa kwa mfumo wa nukta nundu ili kuwawezesha watu wasioona kukisoma baada ya kukizindua jana jijini Dar es Salaam. PICHA: HALIMA KAMBI

Alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana katika hafla ya kutoa Tuzo za I Can zinazotolewa kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu ambao wamepata mafanikio kwenye nyanja mbalimbali za maisha.

Tuzo hizo zinaandaliwa na Taasisi ya Dk. Reginald Mengi People With Disabilities Foundation.

Makamu wa Rais alisema: "Ndugu zangu, hapa leo (jana) naona tuna watu wenye ulemavu kutoka maeneo mbalimbali nchini, sasa niwaombeni kuunda taasisi zenu zisimame vizuri na hasa pale ambapo mfuko wenu wa ruzuku tutakapokuwa tumeumaliza.

"Niwakumbushe pia watendaji wa serikali wakiwamo maofisa ustawi wa jamii, kusimamia mambo ambayo serikali kuu inafanya kwa ajili ya kupunguza mzigo wa maisha kwa watu wenye ulemavu ili yawafikie na kutekelezwa."

Makamu wa Rais alisema serikali ilipitisha Sheria ya Fedha inayoziagiza halmashauri kutenga asilimia mbili ya bajeti kwa ajili ya watu wenye ulemavu ambalo ni kundi maalum, lakini halmashauri hazijachangamka katika kutekeleza maagizo hayo.

“Halmashauri zetu hazijachangamka kutekeleza hili, lakini niwahakikishie kwamba tutasimamia ili kila halmshauri itenge kiasi hicho. Nataka niwaambie mfano mzuri nilioukuta pale Kahama, Halmashauri ya Mji Kahama inatoa fedha hizo na zimefikia Sh. milioni 18 zilizoingizwa, zinazoshughulikiwa na watu wenye ulemavu na jumuiya yao ndiyo inagawa fedha hizo," Makamu wa Rais alisema.

Samia pia alizitaka benki zenye mkono wa serikali ikiwamo CRDB, NMB na Benki ya Posta, kuwa na madirisha maalum ya kutenga fungu litakalokwenda kwa kundi la watu wenye ulamavu ili kuwasaidia kujiajiri na kuondoa fikra iliyopo ndani ya jamii kwamba watu wenye ulemavu hawajiwezi.

Alisema serikali inatambua changamoto mbalimbali zinazowakabili watu wenye ulemavu na tayari imejipanga kuzitatua moja baada ya nyingine ili kuhakikisha wanazimaliza.

Alisema serikali itaajiri walimu 500 mwaka huu walio na ujuzi wa elimu jumuishi ya kufundisha watu wenye ulemavu ambao watawagawa katika shule mbalimbali ili kuwasaidia watu wenye ulemavu.

Alisema serikali pia imekarabati chuo kinachofundisha watu wenye ulemavu mkoani Arusha ili kuandaa walimu maalum kwa ajili ya kusaidia kundi hilo.

“Lengo la serikali ni kuhakikisha haiachi mtu nyuma, tunataka tuhakikishe tunaweka mazingira wezeshi kwa makundi yote na tumejipanga kutatua changamoto moja baada ya nyingine zinazowakabili," Makamu wa Rais alisema.

Samia alipongeza juhudi zinazofanywa na Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, kusaidia watu wenye ulemavu.

“Dk. Mengi ametoa ahadi ya kujenga kiwanda kitakachotoa fursa ya ajira kwa wingi kwa watu wenye ulemavu kufanya kazi kwenye kiwanda hicho. Naomba tumpongeze, tumwombee Mungu amsaidie aweze kutekeleza yale yaliyo moyoni mwake.

"Na leo hii tumeshuhudia akigawa vitabu ambavyo vimeandikwa kwa nukta nundu na vingine vitasambazwa kwenye taasisis za elimu na vyuoni. Tumshukuru sana na anayafanya haya kutimiza yale aliyotuahidi na aliyotuasa katika kitabu chake cha I Can, I Must, I Will," Samia alisema.

Alisema kitabu hicho amekiandika mwenyewe ili kila mtu aelewe alianzia wapi, alikwama wapi, akanyanyuka na mpaka leo anaitwa Dk. Mengi anayemiliki kampuni nyingi.

Alisema serikali itaendelea na utambuzi wa familia zenye watu wenye ulemavu kwa lengo la kukidhi mahitaji ya kielimu kabla ya kuandikishwa.

Aliiomba jamii iendelea kufichua watu wenye ulemavu ambao wanafichwa na kunyimwa haki zao ikiwamo elimu kutokana na imani potofu ndani ya jamii.

Aliagiza kuendelea na kazi ya kuzitambua familia za wenye ulemavu ili kusaidia serikali kupanga mikakati ya kusaidia kundi hilo.

Akizungumza wakati hafla ya chakula iliyoandaliwa na Dk. Mengi kwa ajili wa watu wenye ulemavu jana, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu), Stella Ikupa, alisema Dk. Mengi ameonyesha moyo wa kuwasaidia wahitaji hao kwa muda mrefu na anashirikiana kwa karibu na ofisi yake.

Katika hafla hiyo, Dk. Mengi alisema miaka 25 tangu waanze kukutana na watu wenye ulemavu ni mingi huku akisisitiza kuwa Mwenyezi Mungu akimjalia, ataendelea kufanya hivyo kila mwaka.

Alisema dawa pekee ya kutibu ulemavu si fedha, bali upendo na ili kuwasaidia, ni lazima kuwe na upendo wa kweli.

“Lazima tuwe na upendo wa kweli kutibu ulemavu. Watu wenye ulemavu wana changamoto nyingi. Kwa mfano, umasikini, lakini hatuwezi kupinga umasikini kwa maneno tu, ni lazima tuwasaidie kwa vitendo sababu moja ya kufanya hivyo ni kuzungumzia uwezo wao. Ndiyo maana nikaandika kitabu cha I Can, I Must, I Will, na naomba Mungu awasidie sana," Dk. Mengi alisema.

“Ukiniuliza ni nani hasa rafiki yangu wa kweli, nitasema ni nyie rafiki zangu watu wenye ulamavu," Dk. Mengi aliongeza.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Reginald Mengi, Persons With Disabilities Foundation. Dk. Shimmimana Ntuyabaliwe, alisema taasisi hiyo ina miezi sita tangu kuanzishwa kwake.

Taasisi hiyo ilianzishwa kutokana na agizo lililotokewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mwaka jana, lengo likiwa kuendeleza dira ya Dk. Mengi juu ya ustawi wa watu wenye ulemavu na kutunza historia yake nzuri katika kusaidia makundi maalum hususani watu wenye ulemavu nchini.

Aliongeza kuwa taasisi hiyo pia imeanzishwa kwa lengo la kushawishi watu wenye ulemavu pamoja na watanzania kubadili mtazamo na fikra potofu kwa watu wenye ulemavu.

Alisema taasisi hiyo inakumbana na changamoto moja kubwa ya kumtegemea Dk. Mengi pekee katika kuendesha miradi yake.

“Tunaamini kwamba bado tutaendelea kujiweka sawa ili tushirikiane na wadau wengine wengi katika kuendeleza uwezo wa taasisi yetu na kupanua wigo kuwafikia watu wengi zaidi wenye mahitaji katika jamii ya kundi hili," Dk. Ntyuyabalile alisema.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alisema Dk. Mengi ana jicho la kimungu na ndiyo maana amefanikiwa kwa kiwango kikubwa kuendelea kutoa msaada kwa makundi mbalimbali ya watu wenye ulemavu.

Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, alisema moyo unaoonyeshwa na Dk. Mengi katika kusaidia watu ni wa kipekee na unapaswa kuungwa mkono na kila mmoja.

Katika hafla hiyo, washindi wa nafasi za kwanza walikabidhiwa tuzo, cheti na zawadi ya Sh. milioni mbili kila mmoja.

Vipengele vilivyoshindanishwa ni pamoja na tuzo ya mafanikio katika elimu (wanawake na wanaume), tuzo ya mafanikio ya ujasiriamali, tuzo ya mafanikio katika michezo na tuzo ya ujuzi na mafanikio ya kipekee.

Nyingine ni tuzo ya sanaa na burudani, tuzo ya kujitolea kwa jamii, tuzo ya mafanikio katika uongozi na tuzo ya mafanikio katika siasa.

Pia kulitolewa tuzo ya heshima kwa Dk. Mengi ambayo alikabidhiwa na Makamu wa Rais huku Dk. Mengi alimtunuku tuzo ya heshima Rais John Magufuli kutambua mchango wake kwa kundi la watu wenye ulemavu.

Habari Kubwa