Mfumo kudhibiti wabunge watoro

28May 2020
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Mfumo kudhibiti wabunge watoro

SPIKA Job Ndugai amesema katika kuimarisha mahudhurio ya wabunge bungeni pamoja na ulinzi, umefungwa mfumo maalum wa utambuzi kwa wabunge watakaokuwa wanaingia ndani ya viwanja vya Bunge.

Amesema mfumo huo utaweza kumtambua mbunge kwa sura tofauti na sasa wanapoweka saini kwa alama ya dole gumba.

Aliyasema hayo juzi bungeni kabla ya kuahirisha vikao vya bunge na kueleza kuwa Bunge limeshafunga mfumo huo ambao utatambua wabunge waliohudhuria na watu walioingia bungeni.

“Unajua mambo ya ku-log in kumekuwa na changamoto zake, hata hivyo katika kuimarisha mifumo bungeni, umefungwa mfumo mpya wa Facial, kwenye kila mlango wa bunge hivyo siku zijazo hakutakuwa na changamoto kwa wabunge ambao hawahudhurii,” alisema Ndugai.

Mbali na taarifa hiyo, Spika Ndugai aliwataka wabunge kutopeleka maombi ya msamaha wa kodi ya magari kwa sababu mchakato huo ulishamalizika muda wake na mfumo kufungwa.

“Kama kuna wabunge wanaomba msamaha wa kodi kwenye magari wanayoagiza, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wamelijulisha Bunge kuwa muda wa kufanya hivyo umeisha na mfumo umefungwa,” alisema Ndugai na kuongeza:

“Hivyo msituletee tena maombi hayo, tumalizie muda uliobaki vizuri maana ni mdogo, msituletee maombi ya msamaha wa kodi ya magari, tusubiri kuomba kura kama mtarudi mtaanza nayo kuanzia Novemba,” alisema Spika Ndugai.

YEYE SIYO MKOROFI

Aidha, Spika Ndugai aliwaeleza wabunge kuwa yeye siyo mgomvi kama watu wanavyodhani, na kwamba huwa mkorofi hadi mtu amchokoze kwa makusudi.

Kauli hiyo aliitoa wakati akimsifia Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, kutokana na kazi nzuri anayofanya tofauti na aliyepita.

“Awali kulikuwa na mambo ya kudharauliana, na kwa bahati nzuri mbivu na mbichi zimeonekana na haiwezekani kuwapo watu wa ovyo ovyo.

“Ni sehemu ya miaka mitano, lakini kelele, uongo mwingi kwa kuwa mwisho wa siku lazima Bunge liheshimiwe… watu wengine hawanifahamu vizuri, mimi siyo mgomvi ukiona naparangana na mtu ujue kanichokoza, ukifanya hivyo makusudi utaona,” alisema Spika Ndugai.

Habari Kubwa