Mfumo mpya utoaji leseni, utavutia wawekezaji sekta ya mawasiliano

03Aug 2021
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mfumo mpya utoaji leseni, utavutia wawekezaji sekta ya mawasiliano

MWISHONI mwa wiki iliyopita, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imeanza kutumia mfumo mpya wa maombi ya leseni kwa kundi la leseni kubwa na ndogo.

Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile.

Mfumo huo utamuwezesha muombaji wa leseni kuwasilisha maombi yake ya leseni kwa mamlaka hiyo bila kulazimika kufika ofisini na kukutana ana kwa ana na maofisa wa leseni. 

Mfumo huo laini wa maombi ya leseni (License Management System) umezinduliwa Jumamosi iliyopita  na mawari wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dk. Faustine Ndugulile na Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, ambao wizara zao zinasimamia sekta za Mawasiliano na Utangazaji kupitia TCRA. 

Mkurugenzi wa Leseni na Ufuatiliaji TCRA, John Daffa, akizungumzia mfumo huo mpya ambao ni www.tcra.go.tz, anasema utasaidia kuongeza ufanisi wa upatikanaji leseni kwa wateja wanaonuia kutoa huduma za mawasiliano na utangazaji.

Anasema pia utasaidia kurahisisha mchakato wa mteja kupata huduma za leseni kwa muda mfupi.

Anasema utaokoa gharama za ufuatiliaji kwa mwombaji mpya wa leseni au anaetaka kuhuisha leseni yake na utaongeza ufanisi kwa pande zote mbili yaani mamlaka inayotoa leseni na mwombaji.

Daffa anasema mfumo huo, utaongeza uwazi kwa kuwa utamuwezesha mwombaji wa leseni kupata mrejesho moja kwa moja kwenye simu yake ya kiganjani au kupitia barua pepe juu ya hatua zote na maendeleo ya uchakataji wa leseni aliyoomba na kumwezesha mwananchi kuendelea na shughuli za maendeleo badala ya kufuatilia leseni.

“Tumedhamiria kutoa huduma iliyotukuka kwa kutumia njia ya teknolojia itakayorahisha kazi kwa watumishi wa mamlaka na waombaji wa leseni,” anasema Daffa.

Anafafanua zaidi kuwa, muombaji wa leseni ndogo ataweza kupata leseni yake ndani ya siku tano na leseni kubwa ndani ya siku 45.

Daffa anasema awali mteja alikuwa akitumia zaidi ya mwaka mmoja kupata leseni kutokana na mfumo uliokuwa unatumika.

Anaendelea kueleza kuwa, makundi ya leseni yanayopatikana kwenye mfumo huo ambao mwombaji ataweza kuwasilisha maombi yake bila kulazimika kufika katika ofisi za TCRA ni leseni za pamoja ikihusisha leseni za Huduma ya Maudhui (Content Services) na  Huduma ya Mtandao (Network Services).

Leseni nyingine ni Huduma ya Mifumo Tumizi (Application Services), Miundombinu ya Mtandao (Network Facilities), leseni ya Huduma za Vifurushi na Vipeto, Leseni ya Mtumiaji wa Masafa, Leseni ya matengenezo na Usimikaji, leseni ya Uagizaji Nje na Usambazaji, Rasilimali za Utoaji Namba, leseni ya Huduma za Posta kwa Umma na leseni ya Vifaa Vilivyoidhinishwa.

Anasema hatua ambazo mwombaji wa leseni husika anapaswa kufuata ni pamoja na kutembelea tovuti ya TCRA ambayo ni www.tcra.go.tz kisha kugonga kiunga cha Utoaji Leseni na kisha kubofya kiunga cha Mfumo wa Kuomba leseni ambacho kitampeleka moja kwa moja kwenye ukurasa wenye fomu za kujaza ili aweze kupatiwa leseni anayohitaji kwa ajili ya kutoa huduma za mawasiliano. 

Daffa anasema hatua za maombi ya leseni za mawasiliano kwa kundi la leseni kubwa (Individual License) zitasalia kama ilivyokuwa awali.

 Anasema baada ya mwombaji kuwasilisha maombi yake kupitia mfumo wa maombi ya leseni, itafuata hatua ya kutoa tangazo kwa umma kualika maoni ya wananchi juu ya mwombaji leseni.

Anasema baada ya hatua hiyo, tathmini itafanyika juu ya ombi lililowasilishwa, mwombaji kualikwa kutoa wasilisho la huduma ya mawasiliano anayotarajia kuitoa na kisha hatua ya uidhinishaji leseni na mwisho mteja kupatiwa leseni yake.

Anasema mfumo huo ni mkakati wa serikali kupitia TCRA kurahisisha utaratibu wa upatikanaji huduma za leseni na kuweka mazingira rafiki zaidi kwa wawekezaji katika sekta ya mawasiliano, sekta ambayo inatoa mchango chanya katika ukuaji wa maendeleo ya taifa. 

Waziri Ndugulile, akizungumza kabla ya kuzinduliwa kwa mfumo huo anasema, hadi Septemba Mosi mwaka huu TCRA itakuwa imekamilisha mapitio yote ili wawasilishe kwa Rais kwa ajili ya kuanza kwa utelezaji.

“Tayari tumeshafanya maboresho katika suala zima la utoaji wa leseni lakini bado mnatakiwa kufanya mapitio kwenye tozo na maudhui ya mtandaoni na namna ya kutekeleza lengo ni kuhamasisha uwekezaji mkubwa,” anasema Dk. Ndugulile.

Anafafanua kuwa, awali mfumo huo wa utoaji leseni ulikuwa ukichukua miezi hadi mwaka mmoja kukamilika lakini kwa sasa leseni ndogo hazizidi siku tano na leseni kubwa hazichukui siku 45.

Anasema wizara inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta hiyo ya mawasiliano na teknolojia ili kuzifikia wilaya  69 ambazo hazina redio nchini.

“Kupitia mfumo huu, tunahamasisha wawekezaji kijitokeza sasa kuwekekeza katika sekta ya mawasiliano ili kufikia wilaya zilizoko pembezoni ambazo hazifikiwi na huduma ya mawasiliano,” anasema Dk. Ndugulile.

Anaendelea kusema kuwa, mfamo huo utamuwezesha mteja kufuatilia kila hatua ya utolewaje wa leseni yake na utaongeza uwajibikaji kwa watendaji kwa sababu watakuwa wanaonekana wanavyotekeleza majukumu yao.

“Kupitia mfumo huu tutapunguza sana kukutana lakini pia na yale mambo mengine ya kurahisisha kazi,” anasema.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa, anasema mfumo huo utaondoa urasimu kati ya mteja na mtoa huduma kwa sababu maombi yatafanyika mtandaoni.

Anasema pia mfumo huo utaleta mabadiliko makubwa ya uendeshaji kwa sababu utaongeza weledi na ufanisi kwa wawekezaji kuomba leseni kwa ajili ya uwekezaji kwenye Televisheni na Redio.

“Mfumo huu unatutoa kwenye mfumo wa zamani wa kuwasiliana kati ya mteja na mtoa huduma uso kwa uso na sasa utaratibu utafanyika kwa sayansi na teknolojia na hata yale mambo mengine ya unanisaidiaje (rushwa) hayatakuwapo,” anasema Bashungwa.