Mfumo wa kielektroniki waongeza makusanyo NSSF

21Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Mfumo wa kielektroniki waongeza makusanyo NSSF

MATUMIZI ya mfumo wa kielektroniki wa malipo ya serikali (GePG), katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), umeongeza ukusanyaji wa mapato na kuvunja rekodi ya ukwasi kutoka Sh. Trilioni 3.2 hadi Trilioni 4.4 kwa miaka miwili.

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, William Erio:PICHA NA MTANDAO

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Willium Erio, alisema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mkutano wa kupokea taarifa ya matokeo ya matumizi na tathmini ya mfumo wa GePG, ambao pia umeongeza ukusanyaji wa makusanyo ya michango kutoka kwa wanachama kutoka Sh. bilioni 694 kwa mwaka na kufikia Sh. trilioni 1.1 Juni mwaka huu.

Alisema mfumo huo ulianza kutumika Aprili, mwaka jana, kwa ajili ya kukusanya michango kwa wanachama kutoka sekta rasmi na sekta isiyo rasmi pamoja na kukusanya kodi ya pango kwa wapangaji waliopanga kwenye vitenga uchumi vya shirika hilo.

Aidha, alisema mfumo huo umeliletea shirika mafanikio makubwa ikiwamo kuongeza mapato kutoka kwa wanachama, ambapo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita ilikuwa ni Sh. bilioni 694 kwa mwaka, lakini katika kipindi hiki hadi kufikia Juni 30, mwaka huu, yamekaribia Sh. trilioni 1.1, ongezeko ambalo ni kubwa katika kipindi kifupi lililochangiwa na matumizi ya GePG.

Kwa mujibu wa Erio, mfumo huo umesaidia kuondoa ahadi hewa za malipo, na kwamba kabla ya mfumo huo kulikuwa na akaunti za benki 78, lakini baada ya mfumo huu zimeondolewa na kubaki tatu,

“Kuondoa akaunti nyingi kumepunguza makato kutoka Sh. milioni 9.5 kwa mwezi hadi kufikia Sh. milioni 4 kwa mwezi na umeweka uwazi,” alisema.

“Hii GePG imeleta mabadiliko makubwa pale NSSF, imeongeza thamani ya mfuko kwa zaidi ya asilimia 40 ndani ya kipindi cha miaka miwili ni kutokana na matumizi ya mfumo huu,” alifafanua.

Aidha, alisema mfumo huo umelisaidia sana shirika hilo kwa kuongeza mapato, kupunguza gharama za uendeshaji ambazo walikuwa wanatumia katika matumizi ya kawaida na kuwawezesha kutoa huduma bora zaidi kwa wanachama na kwa wakati.

 

Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, alipongeza shirika hilo na kwamba mashirika mengine yanapaswa kuiga.

Alisema yameongeza kiwango cha makusanyo tangu mfumo huo ulipoanzishwa mwaka 2017, kwamba takwimu za maduhuli yaliyokusanywa mwaka wa fedha 2015/16, serikali ilikuwa inakusanya kwa mwaka maduhuli ya Sh. bilioni 688.7.

Alisema makusanyo yameongezeka kutoka Sh. bilioni 688.7 mwaka 2019/2020, hadi Sh. trilioni 2.699, kwamba katika mwaka huu wa fedha 2020/21, wanatarajia kukusanya zaidia ya kiasi hicho cha fedha.

“Ukiangalia mwaka wa fedha 2015/16 na 2019/20, tumeongeza ukusanyaji wa maduhuli ya serikali kwa asilimia 292 kiasi ambacho ni kikubwa sana,” alisema James.

Habari Kubwa