Mfumo wa kongani wainua wakulima

28Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Mbeya
Nipashe
Mfumo wa kongani wainua wakulima

KITUO cha Kuendeleza Kilimo Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kimesema katika salamu zake za mwaka mpya kwa Watanzania kwamba mafanikio ya taifa katika kuinua kilimo na kupunguza umaskini katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini yametokana na mfumo wa kongani unaotumika katika mikoa ya Iringa-

WAKULIMA

Njombe, Mbeya na Songwe.

Akiwasilisha salamu hizo kwa Watanzania, Afisa Mtendaji Mkuu wa SAGCOT, Geoffrey Kirenga, alisema, taasisi yake mwaka 2010 ilipewa jukumu la kuboresha maisha ya wakulima na kuongeza tija katika kilimo ili kuirudishia mikoa ya nyanda za juu kusini hadhi yake kuzalisha chakula kwa ajili ya taifa na hata kuuza nje.

 

Ili kufikia lengo hilo, Kirenga aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa Sagcot ilibuni ya mfumo wa kongani ambao  umesaidia sana kuwakomboa wakulima kwa kuainisha mazao ya kipaumbele na kuyafanyia kazi kwa kuinua tija katika uzalishaji.

 

“Siri ya mageuzi makubwa yaliyopatikana ni mfumo wa kongani ambao tumeubuni na kuusimamia kwa karibu sana kwa sababu ni mfumo shirikishi. Iwapo utatumika katika maeneo mengine ya nchi kama wanavyohitaji wanachi wengi, sekta ya kilimo nchini itapiga hatua katika uzalishaji,” alibaini Kirenga.

 

Kongani zinazofanyakazi Nyanda za Juu Kusini ni Kongani ya Ihemi (mikoa ya Iringa na Njombe), Kogani ya Mbarali (Mbeya na Songwe) na Kongani ya Kilomberoa ambayo ilizinduliwa mwishoni mwa mwaka jana itahudumia wananchi wa Mkoa wa Morogoro na wilaya zake zote.

 

Alisema SAGCOT ina nia ya kufungua kongani nyingine ndani ya ukanda wa Nyanda za Juu Kusini ili kunufaisha

wananchi katika maeneo ya Ludewa, Rufiji na Sumbawanga na kuikuza sekta ya kilimo ambayo ndiyo kichocheo cha uanzishwaji wa viwanda.

 

“Sekta ya kilimo ndio mzalishaji mkuu wa malighafi ambazo zitachagiza uanzishwaji wa viwanda katika maeneo mengi nchini. Ni wajibu wa kila mdau katika kilimo kuendelea kutoa mchango utakaosaidia kukuza

uzalishaji katika sekta hii,” alisisitiza Kirenga.

 

Kirenga alieleza kuwa katika Kongani ya Ihemi uzalishaji wa nyanya umeongezeka, hivyo Tanzania haiagizi tena nyanya kutoka nje, viwanda viwili vikubwa vya kusindika nyanya vya Dabaga na Darsh Industries vimeanzishwa mkoani Iringa na sasa lipo soko la uhakika la zao la nyanya.

 

 Viwanda hivyo vina uwezo wa kusindika tani mia mbili za nyanya kila siku na kutengeneza bidhaa mbalimbali zinazotokana na nyanya.

 

Alieleza kuwa SAGCOT ina shauku ya kuona mikoa mingine inaitumia mikoa yenye kongani tayari kama darasa kujifunza namna mfumo huu unavyofanya kazi na kuutumia ili kuchochea ukuaji wa sekta ya kilimo.

 

“Uhitaji wa elimu kupitia mfumo wa kongani ni mkubwa katika kanda nyingine za nchi yetu, hivyo tutaendelea kutoa elimu kwa kushirikiana na serikali pamoja na sekta binafsi ili kuongeza tija katika kilimo na kuyaboresha maisha ya wananchi,” alisema Kirenga.

 

 

 

 

Habari Kubwa