Mfumuko wa bei umebaki asilimia 3

08Mar 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Mfumuko wa bei umebaki asilimia 3

OFISI ya Taifa ya Takwimu (NBS) imesema mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Februari 2019 umebaki kuwa asilimia 3 kama ilivyokuwa kwa mwaka ulioishia mwezi januari mwaka huu.

Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Kijamii, Ephraim Kwesigabo.

Akizungumza leo jijini hapa, Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Kijamii, Ephraim Kwesigabo, amesema kuwa hali hiyo imetokana na kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa Februari mwaka huu kubaki kama iliyokuwepo Januari mwaka huu.

Amesema mfumuko wa bei wa taifa unapima kiwango cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zinazotumiwa na kaya binafsi.

Kwesigabo amefafanua hali hiyo imechangiwa na kuongezeka na kupungua bei za baadhi za bidhaa za vyakula na bidhaa zisizokuwa za vyakula kwa kipindi kilichoishia Februari mwaka huu.

Amezitaja bidhaa za vyakula zilizopungua bei ni mchele (3.0%), unga wa mahindi (6.4%), mtama (5.1%) unga wa muhogo (6.9%), maharage (4.5%) na viazi vitamu vilivyoshuka bei kwa asilimia (8.2%).

Kadhalika amezitaja pia biadhaa zisizokuwa za vyakula ambazo bei zimepanda ni pamoja na mavazi (2.7%), mkaa (10.1%), majokofu (2.1%) na gharama za kumuona daktari kwenye hospitali binafsi kwa asilimia 4.6.

Habari Kubwa