Mfumuko wa bei wabaki pale pale

09Jul 2020
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Mfumuko wa bei wabaki pale pale

MFUMUKO wa bei wa Taifa, kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2020 umebaki kuwa asilimia 3.2 kama ilivyokuwa kwa mwaka unaoishia mwezi Mei, 2020.

Kaimu Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ruth Minja, picha mtandao

Hayo yalibainishwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Sensa na Takwimu za Jamii wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Ruth Minja, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Minja, alisema kutokana na hali hiyo, inamaanisha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia Juni, 2020 imebaki kuwa sawa na kasi iliyokuwapo kwa mwaka ulioishia Mei, 2020.

“Mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Juni, 2020 kuwa sawa na mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia mwezi Mei 2020 kumechangiwa na kuongezeka na kupungua kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia mwezi Juni, 2020 zikilinganishwa na bei za mwezi Juni, 2019,” alifafanua Minja.

Pia, alisema baadhi ya bidhaa za vyakula zilizopungua bei kwa Juni, 2020 zikilinganishwa na bei za Juni, 2019 ni pamoja na unga wa mahindi kwa asilimia 1.6, matunda kwa asilimia 2.1,viazi mviringo kwa asilimia 5.0 na mihogo kwa asilimia 13.3.

“Kwa upande mwingine, baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizoongezeka bei kwa Juni ,2020 zikilinganishwa na bei za Juni 2019 ni pamoja na mavazi kwa asilimia 2.7,gesi ya kupikia kwa asilimia 7.8, mkaa kwa asilimia 11.2, samaki kwa asilimia 2.7 na vitabu vya shule kwa asilimia 1.5,’” alisema Minja.

Vile vile, alisema mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia Juni,2020 umepungua hadi asilimia 3.8 kutoka asilimia 4.4 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei,2020.

Habari Kubwa