Mfungwa aliyesamehewa adaiwa kuiba

12Dec 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Mfungwa aliyesamehewa adaiwa kuiba

SIKIO la kufa halisikii dawa. Ndivyo inavyoweza kuelezwa baada ya mfungwa  aliyeachiwa kwa msamaha wa Rais John Magufuli wakati wa maadhimisho ya Uhuru,  kukamatwa kwa tuhuma za wizi zikiwa zimepita saa nane tangu alipotoka gerezani.

Mfungwa Mussa Msola akiwa chii ya Ulinzi wa Polisi.

Mfungwa huyo, Musa Msolwa, maarufu kama Hitler, ambaye aliachiwa juzi saa 11:00 jioni Gereza la Makambako mkoani Njombe, na ilipofika saa 9:00 usiku akiwa mtaani, aliamua kwenda kwenye nyumba ya kulala wageni ya Nang’ano na kuvunja ili kujipatia fedha.

Akisimulia tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Njombe, Kamishna Msaidizi (ACP) Khamis Issa, alisema Msolwa baada ya taratibu zote za kutoka gerezani kufanyika, alikuwa mfungwa wa kwanza kushukuru kitendo cha Rais kuwaachia kwa msamaha.

“Wakati akishukuru alisema walizoea kufanya wizi wakienda mtaani wasiende kuiba na aliomba serikali isaidie kujengwa Mahakama Kuu ya Njombe,” alisema.

Kamanda Issa alisema mfungwa huyo aliwaeleza kuwa baada ya kwenda mtaani na kukosa kwa kwenda kwa sababu hana maelewano mazuri na baba yake, aliendelea kurandaranda huko.

“Ameeleza kuwa baada ya kurandaranda mtaani na kukosa kwa kwenda, ilipofika saa 9:00 usiku, aliingiwa na tamaa akaamua kwenda kwenye hiyo nyumba ya kulala wageni ili kuiba,” alisema.

Kamanda Issa alisema baada ya kufika hapo, alichungulia na kuona watu wamelala ndipo alipovunja na alipoingia ndani, alimwona mmoja wa wanawake waliokuwamo akiwa na fedha.

“Alipoziona hizo fedha na akiwa katika harakati za kwenda kuziiba, ndipo waliolala waliposhtuka na yeye katika kujihami aliwataka wajifunike sura zao kwa nguo walizokuwa wamejifunikia.

“Ndani ya nyumba hiyo ya kulala wageni kulikuwa na wahudumu, walinzi na baadhi ya wageni ambao walipiga kelele na kupata msaada kutoka kwa majirani ambao walifika hapo na kumkamata kisha kumpiga,” alisema.

Katika tukio hilo, alisema Msolwa alijeruhiwa kwa panga eneo la kichwani na jana alipelekwa hospitalini kwa matibabu.

Alisema katika msamaha huo wa Rais Magufuli aliachiwa akiwa na kosa la uvunjaji ambalo ndilo alilolirudia baada ya kuachiwa huru.

Habari Kubwa