Mfungwa aliyegoma kuondoka gerezani ana matatizo ya akili

11Dec 2019
Nebart Msokwa
Mbeya
Nipashe
Mfungwa aliyegoma kuondoka gerezani ana matatizo ya akili

JESHI la Magereza mkoani Mbeya, limethibitisha kuwa mfungwa Merard Abraham ambaye aligoma kuondoka gerezani baada ya kutolewa kwa msamaha wa Rais John Magufuli wakati wa Sherehe za Uhuru wa Tanzania ana matatizo ya afya ya akili.

Mkuu wa Jeshi la Magereza wa Mkoa wa Mbeya, Mathias Mkama akizungumza na wandishi wa habari kuhusu mfungwa aliyegoma kutoka gerezani baada ya kutakiwa kutoka kwa msamaha wa Rais.

Akizungumza na wandishi wa Habari ofsini kwake jana, Mkuu wa Jeshi la Magereza wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Magereza, Mathias Mkama amesema kijana afya yake ilikuwa inabadilika mara kwa mara.

Amesema pamoja na kwamba alionekana kugoma kuondoka gerezani hapo lakini ndugu zake walienda kumchukua na wakaondoka naye kwenda Mwakaleli wilayani Rungwe na kwamba Jeshi hilo liliwasaidia baadhi ya gharama za usafiri.

Mkama amesema awali alienda ndugu yake mmoja kwa ajili ya kumchukua lakini baada ya kubaini kuwa ni ‘mtata’ akaamua kuwasiliana na ndugu wengine na hivyo wakaja wengi na wakafanikiwa kumchukua.

“Kwa sababu alikuwa amejijeruhi kwa jiwe kwenye paji la uso, tulilazimika kumtibu kwanza kwenye zahanati yetu na baada ya kuchunguzwa matatizo mengine wataalamu wetu walithibitisha kuwa yuko vuizuri na hivyo tukaruhusu aondoke,” amesema Mkama.

Amesema wafungwa wote 259 wa walionufaika na Msamaha wa rais walishachukuliwa na ndugu zao na kurejea nyumbani baada ya Jeshi hilo kuwapatia nauli ya kuwarudisha kila mmoja nyumbani kwao.

Kamanda Mkama amesema Merard amekuwa anataja kuwa anataka kurudi katika Gereza la Ukonga jijini Dar es salaam kwa sababu ndiko alikokuwa amehukumiwa kwenda kwa mara ya kwanza na kwamba alitumikia kifungo kwa mara ya kwanza katika gereza hilo kabla ya kuhamishiwa Mbeya.

Aidha amesema kitendo cha kijana huyo kutamani abaki gerezani ni haki yake ya kuzungumza ambayo kila mtanzania anayo kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania na hivyo wasingeweza kumchukulia hatua yoyote kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kwa kusimamia zoezi la kuwarejesha raia ambao waliachiwa kwa msamaha wa Rais katika Magereza ya Ruanda pamoja na gereza la kimkakati la Kilimo la Songwe.

Jana wakati wa utekelezaji wa agizo hilo la Rais, Merard alikataa kutoka gerezani hapo kwa madai kuwa hana mahali pa kwenda na hivyo akataka badala ya kurejeshwa nyumbani apelekwe katika Greza la Ukonga jijini Dar es salaam.

Wakati wa sherehe za kuadhimisha Uhuru wa Tanganyika zilizofanyika katika Mkoa wa Mwaza, Raid Dk. John Magufuli alitangaza msamaha kwa wafungwa 5533 ambapo katika Mkoa wa Mbeya, walinufaika wafungwa 259.

Habari Kubwa