Mganga Mkuu Mkoa awataka wananchi kupata chanjo corona

21Oct 2021
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Mganga Mkuu Mkoa awataka wananchi kupata chanjo corona

MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Dk. Silvia Mamkwe, amewasihi wananchi kujitokeza kuchanja chanjo ya kujikinga na maambukizi ya Uviko-19, ili wajihakikishie usalama wa afya zao.

Aidha, amewataka kuepuka propoganda za kuwa chanjo hiyo haifai ina madhara kwa binadamu na kugandisha vyuma ukipita.

Aliyasema hayo jijini Arusha, wakati akitoa nasaha zake katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Jiji hilo.

“Chanjo hii ni muhimu na imefanyiwa tafiti za kisayansi na serikali imejiridhisha. Mkichanja hata ukipata Uviko-19 hautaumwa kama yule ambaye hajachanjwa, hivyo ujanja kuchanja," alisema.

Alisema kwa watu wasiochanja wakipata maambukizi matibabu yale yanachukua muda nakusababisha gharama kwa familia na kwa mgonjwa.

"Lakini hapa unaweza usipone sababu inakuwa kubahatisha na itategemea umepata maambukizi kwa kiasi gani sasa kuliko kukaa kusubiri kufikia hatua hii bora tukachanje," alisema.

Alisema hata baadhi ya propoganda kama za kuganda damu mwilini kwa sababu ya kupata chanjo hiyo wao kama wataalamu walifuatilia na kubaini uzushi wa baadhi ya watu, kwamba hakuna tukio lolote la mtu kuganda.

Alisisitiza kuwa ni vyema watu wakafuata ushauri wa kitaalamu na kusikiliza wanasayansi na siyo kila mtu au kufuata mitandao.

Habari Kubwa