Mganga, mwanawe mbaroni wakituhumiwa kwa ubakaji

22Oct 2017
Elisante John
Nipashe Jumapili
Mganga, mwanawe mbaroni wakituhumiwa kwa ubakaji

JESHI la Polisi mkoani Singida linamshikilia mganga wa tiba asilia, Daud Ali, maarufu kama Karatu Babu (74) na mwanawe Abdallah Yahya (31) maarufu kama Kola, ambaye ni dereva wa magari, kwa tuhuma za kuwabaka watoto 14 wa shule za msingi.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Isaya Mbughi.

Watuhumiwa hao ni wakazi wa mtaa wa Unyankindi tarafa ya Mungumaji, wote wakiwa wapangaji kwenye moja ya nyumba iliyoko karibu kabisa na Shule ya Msingi Unyankindi, Manispaa ya Singida.
 
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Isaya Mbughi, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa watoto hao ni wanafunzi katika shule tofauti katika manispaa hiyo.

Alisema mganga huyo na mwanawe walikuwa wanatumia ubunifu wa hali ya juu katika kufanikisha njama zao ikiwamo kuwaonyesha watoto picha za video kupitia kompyuta mpakato na kuwapatia pipi kisha kuwabaka.
 
Mbughi alisema wakati mtoto wa mganga huyo akiendelea kuonyesha picha, baba yake huwaingiza chumbani watoto wa kike mmoja baada ya mwingine na wakikanyaga kitambaa chekundu kilicholoanishwa maji, hupoteza fahamu.
 
Alibainisha kuwa mganga huyo hubaka mtoto mwenye umri mkubwa kidogo lakini wale wadogo huchezewa na wanapozinduka hupakwa dawa nyeupe kwenye paji la uso na kuamrishwa wasimweleze mtu yeyote vinginevyo watakufa.
 
Kamanda Mbughi alisema watuhumiwa wanadaiwa kutenda kosa hilo tangu Desemba, mwaka jana, hadi Oktoba, mwaka huu, huku hadi Oktoba 16, tayari watoto 14 wamelalamika kubakwa na mganga huyo.
 
Alisema watoto hao licha ya kupatiwa pipi na kuonyeshwa picha za video, walikuwa wakipewa fedha kati ya Sh. 200 na 2,000 kama zawadi kwa tendo hilo.
 
Alisema baada ya watuhumiwa kutiwa nguvuni, walipopekuliwa ndani ya makazi yao, ulipatikana ushahidi wa pipi ambazo zilikuwa zinatumika kuwapa watoto.
 
Aidha, Mbughi alisema katika uchunguzi, jeshi hilo lilifika katika shule wanazosoma watoto hao (majina yanahifadhiwa) na kwa kushirikiana na daktari na watoto watoto 12 kati ya 14 waliolalamika, walibainika kuingiliwa kimwili.

Mbughi alisema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote kujibu mashitaka ya kubaka, shambulio la aibu na njama za kutenda kosa.

Habari Kubwa