Mghwira kuzikwa mkoani Arusha leo

26Jul 2021
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe
Mghwira kuzikwa mkoani Arusha leo

ALIYEWAHI kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, anatarajiwa kuzikwa leo nyumbani kwake, Makumira wilayani Arumeru mkoani hapo.
 

Kwa mujibu wa msemaji wa familia ambaye ni mdogo wa marehemu, Helen Mghwira, wanasumbiri mtoto mkubwa wa marehemu, Fadhili Mgwira, ambaye anafanya kazi nchini Uingereza.
 
"Dada yetu Anna tutamzika hapa hapa nyumbani kwake Makumira na kwa sasa tunaendelea na taratibu za maandalizi wakati tukimsubiri mtoto mkubwa wa marehemu Wakili Fadhili," alisema.
 
Alisema familia imepata pigo kubwa la kuondokewa na mwanafamilia ambaye alikuwa na upendo wa dhati kwa wanafamilia aliyetaka kuona watoto wa jamii inayomzunguka anapata elimu haswa kwa watoto wa kike.
 
"Dada alikuwa mchapa kazi mwenye moyo wa upendo na kutaka kuona kila mtoto kwenye jamii inayomzunguka anapata elimu kwa wakati," alisema.
 
Alisema licha ya upendo wake huo, marehemu alikuwa ni mtu wa msimamo ambaye alikuwa akiamua jambo lake ameamua na ni lazima alisimamie litekelezeke.
 
Kuhusu kifo cha Anna, alisema kimekuwa cha ghafla kwa sababu ameugua muda mfupi lakini hakuwa amezidiwa kiasi cha kupoteza maisha. 
 
Alisema marehemu alianza kuugua Jumatano ya wiki iliyopita ambapo walimpeleka Hospitali ya Nkaoaranga inayomilikiwa na Kanisa la Kinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Meru na kupatiwa matibabu ya kwenda na kurudi nyumbani. 
 
Alisema Jumamosi hali yake ilibadilika na kupeleka Hospitali ya Rufani ya Mkoa ya Mount Meru, ambapo alifanyiwa vipimo na kubainika kwamba alikuwa na anasumbuliwa na limonia kali. 
 
"Baada ya kulazwa aliendelea na matibabu lakini alikuwa hapendi kula lakini juzi kabla ya kufikwa na mauti alikuwa anakula vizuri, ambapo alisema anatamani kurudi nyumbani lakini ghafla hali yake ilibadilika na kuhamishiwa chumba cha wagonjwa mahututi na baada ya muda mfupi alifariki," alisema.