Mgodi wa Almasi Mwadui wasitisha uzalishaji madini

26Jul 2021
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Mgodi wa Almasi Mwadui wasitisha uzalishaji madini

MGODI wa uchimbaji madini ya Almasi (Williamson Diamond LTD), uliopo Mwadui wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, umeelezwa kusitisha uzalishaji wa madini hayo, sababu ya kuathiriwa na janga la virusi vya corona.

Naibu Waziri wa madini Prof.Shukrani Manya akizungumza kwenye ufunguzi wa maonesho ya Biashara na Teknolojia ya madini mkoani Shinyanga.

Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya, amebainisha hayo jana kwenye ufunguzi wa maonesho ya Biashara na Teknolojia ya Madini mkoani Shinyanga, kwa niaba ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Alisema kutokana na janga la virusi vya corona kuendelea kupamba moto, kumesababisha mgodi wa uchimbaji madini ya Almasi Mwadui, kusitisha uzalishaji wa madini hayo.

 “Mgodi wa Mwadui wa uchimbaji madini ya Almasi uliathiriwa sana na corona, na kusababisha kusitisha uzalishaji wa madini, lakini  mwezi ujao Agosti wataanza tena shughuli za uchimbaji madini,”alisema Prof Manya.

Katika hatua nyingine alisema Mkoa wa Shinyanga nao upo mbioni kuanzishwa kiwanda cha kusafisha dhahabu, kama ilivyo katika Mikoa ya Mwanza, Geita, na Dodoma, ili kuyaongezea thamani madini na kuzalisha ajira, badala ya madini ghafi kusafirishwa katika nchi nyingine.

Rais wa chama cha wachimbaji wadogo Tanzania (FEMATA)John Bina, akizungumza kwenye maonesho hayo ya Biashara na Teknolojia ya madini mkoani Shinyanga.

Aidha Prof Manya alisema, Serikali itaendelea pia kuwa boreshea mazingira rafiki wachimbaji wadogo, kwa kuwatengea maeneo ya uchimbaji madini yaliyofanyiwa utafiti wa Kijiolojia, ili wafanye uchimbaji wenye tija na kuacha kuchimba madini kwa kubahatisha.

Pia amewatahadharisha wanunuzi wa madini, waache kununua madini hayo nje ya mfumo wa Masoko ya madini, ili kuepuka kuuziwa madini feki, ambapo kwenye masoko hayo biashara zake hufanyika kwa uwazi.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati akizungumza kwenye ufunguzi wa maonesho ya Biashara na Teknolojia ya madini mkoani humo.

Kwa upande wake Rais wa chama cha wachimbaji  wadogo hapa nchini (FEMATA) John Bina, aliiomba Serikali ione namna ya kuwawezesha mafundi mchundo kupata mafunzo nje ya nchi, ili kuwawezesha kujifunza kuhusu Teknolojia bora, ambazo zitawasaidia wachimbaji wadogo kupata Teknolojia rahisi na kuendeleza shughuli zao.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati, alisema maonesho hayo yatakuwa chachu katika mkoa huo, na kuongeza ukusanyaji mapato yatokanayo na rasilimali madini, pamoja na wachimbaji wadogo kupata ujuzi zaidi kutoka kwa wachimbaji wakubwa, wakiwamo na wafanyabiashara kubadilishana uzoefu na kuongeza mtandao.