Mgodi wa Geita watumia bil. 10/- shule wasichana

11Mar 2017
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe
Mgodi wa Geita watumia bil. 10/- shule wasichana

KATIKA kuthamini mchango wa mwanamke mkoani Geita, Mgodi wa dhahabu wa Geita (GGM), imesaidia shule ya bweni ya wasichana Nyankumbu kwa kuwekeza mradi wa Sh. bilioni 10.

waziri wa elimu, profesa joyce ndalichako.

Shule hiyo ina vifaa vya kisasa vya sayansi kwenye maabara zake za Fizikia, Kemia na Baiolojia. Pia vifaa vya maabara ya somo la kompyuta, nyumba za walimu 36, maji na ukuta mkubwa wa kuzunguza eneo lote la shule hiyo.

Meneja Mawasiliano na Mahusiano wa GGM, Tenga Tenga, alisema GGM pia imeanzisha miradi mbalimbali mkoani Geita ambayo imelenga kuwawezesha wanawake katika kujinyanyua kiuchumi, kijamii na kielimu.

Alisema shule hiyo ya sekondari yenye madarasa 21, ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 900 lengo kuu ni kuhakikisha wasichana wanapata kiwango bora cha elimu, hususan wasichana kutoka katika jamii ya wakazi wa Geita.

Tenga alisema mbali na shule hilo, pia GGM imeweza kusaidia mradi wa usambazaji maji kwa wakazi zaidi ya 130,000 wa Geita.

Alisema GGM pia imesaidia mradi wa kuzuia malaria kwa kina mama, wanawake na wajawazito kwa wakazi zaidi ya 100,000, na kwamba watoto 17,800 walio chini ya miaka mitano wamenufaika.

Aidha, katika kuwasaidia zaidi wanawake, GGM imesaidia vilevile magari matatu ya kubebea wagonjwa, kila moja likiwa na thamani ya Sh. milioni 40.

“Mradi huu unakwenda sambamba na mradi wa kilimo cha mpunga na alizeti ambapo zaidi ya kaya 4,000 zinanufaika moja kwa moja.

Zaidi ya heka 900 zinalimwa mpunga na alizeti na hivyo kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa chakula cha kutosha, lengo kuu ni kumwezesha mwakamke wa Geita kujinyanyua kiuchumi pamoja na familia zao,” alisema Tenga.

Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yalifanyika Jumatano katika maeneo mbalimbali nchini.

Habari Kubwa