Mgodi wa Mwadui wapandikiza vifaranga vya samaki Bwawa la Mwang'olo

08Dec 2023
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Mgodi wa Mwadui wapandikiza vifaranga vya samaki Bwawa la Mwang'olo

MGODI wa uchimbaji Madini ya Almasi (WDL) uliopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, umepandikiza vifaranga vya Samaki aina ya Sato katika Bwawa Jipya la Mwang'olo, ili kuinua kipato cha wananchi pamoja na kupata kitoweo.

Katibu Tawala wilaya ya Kishapu Fatma Mohamed akipandikiza Vifaranga ya Samaki bwawa jipya ya Mwang'olo.

Zoezi hilo la upandikizaji vifaranga vya Samaki limefanyika leo Desemba 8,2023 kwa kuzinduliwa na Katibu Tawala wa wilaya ya Kishapu Fatma Mohamed akimwakilisha Mkuu wa wilaya ya Kishapu Joseph Mkude.

Meneja Mahusiano Mgodi wa Almasi Mwadui Bernard Mihayo,akizungumza katika zoezi hilo, amesema wametekeleza agizo la Serikali la kurudisha kila kitu ambacho kiliharibika baada ya kupasuka kwa Bwawa la Majitope la Mgodi huo Novemba mwaka jana.

Amesema zoezi la ulipwaji fidia kwa Waathirika, limemalizika, na sasa wanachofanya ni kurudishia Mazingira ikiwamo upandaji miti, na kupandikiza vifaranga vya Samaki katika Bwawa Jipya, ili wananchi waendelee na shughuli zao kama kawaida ikiwamo uvuvi wa Samaki.

"Baada ya kupasuka kwa bwawa la kuhufadhia Majitope, liliathiri Bwawa ambalo wananchi walikuwa akilitumia kufanya shughuli za uvuvi wa Samaki," amesema Mihayo.

"Baada ya kujenga Bwawa hili Jipya katika Kijiji cha Mwang'olo,tumetekeleza Maagizo ya Serikali na Leo tumekuja kupandikiza vifaranga vya Samaki 5,000 aina ya Sato ili wananchi waendeleE na shughuli zao za uvuvi kama zamani," ameongeza Mihayo.

Aidha, amesema katika zoezi la upandaji miti ili kutunza Mazingira katika vijiji vyote vinayozunguka Mgodi huo kwamba hadi sasa wameshapanda Miti 10,000 na zoezi hilo ni endelevu.

Naye Afisa Uvuvi wilaya ya Kishapu Moses Ng'winza, ametoa wito kwa wananchi wasubili hadi miezi Sita Samaki hao watakuwa tayari wamekuwa wakubwa, pamoja na kusubiri maelekezo kutoka Serikalini  na kupewa elimu ndipo waanze shughuli za uvuvi.

Katibu Tawala wa wilaya ya Kishapu Fatma Mohamed, ameupongeza Mgodi huo wa Mwadui kwa kutekeleza Maagizo ya Serikali, na leo wamezindua zoezi la upandikizaji vifaranga vya Samaki.

Amewataka wananchi kulitunza bwawa hilo, na kila mmoja awe mlinzi wa mwezake pamoja na kuacha kulima Kando ya bwawa ili Samaki hao waje kuwa msaada mkubwa kwao kiuchumi na kupata kitoweo.

Nao baadhi ya wananchi hao akiwamo Mvuvi Laurent Fabiani, amesema wanaushukuru Mgodi huo kwa kupandikiza vifaranga vya Samaki katika bwawa jipya, ili warudi katika shughuli zao za uvuvi na kujiongezea kipato, ambapo kwa sasa anaendelea na Kilimo.