Mgogoro ardhi wafukuta

25Nov 2016
Richard Makore
Dar es Salaam
Nipashe
Mgogoro ardhi wafukuta

SAKATA la wakazi wa wilaya za Serengeti na Butiama kugombea mipaka limechukua sura mpya baada ya kuundwa kamati ya kutafuta suluhu ya suala hilo.

waziri wa ardhi nyumba na makazi, wiliam lukuvi.

Mbunge wa Serengeti, Marwa Ryoba (Chadema), aliiambia Nipashe jana kuwa suala hilo kwa sasa limekabidhiwa kwa kamati inayohusisha wataalamu kutoka Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Mgogoro huo pia unahusisha mipaka ya wilaya za Bunda na Serengeti katika maeneo ya Mikomariro, Motilibe, milima ya Bikairi na Metoha.

Mbunge huyo alisema sakata hilo lazima lipatiwe ufumbuzi kabla hakujaibuka madhara ambayo yanaweza kutokana na mapigano ya wananchi kugombea mipaka.

Kwa upande wa mpaka wilaya ya Butima, wakazi wa wilaya hiyo wamevuka na kujenga makazi ya kuishi eneo la wilaya ya Serengeti.

Rioba alisema mgogoro huo usipopatiwa ufumbuzi unaweza kuleta madhara kwa kuwa hivi sasa wakazi wa Bunda na Butiama wamehama na kuvuka mipaka yao na kuingia Serengeti.

Alisema maeneo yote yana mipaka iliyowekwa mwaka 1974 wakati wa kugawa vijiji, lakini wanasiasa ndio waliochangia kuivuruga kwa lengo la kujijenga kisiasa bila kuangalia maslahi ya wapigakura wao ambao awali walikuwa wakiishi na kufanya shughuli zao.

Kuhusu kutembelea wananchi katika vijiji mbalimbali ili kubaini matatizo ya wananchi katika jimbo lake, Ryoba alisema amepanga kufanya ziara kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi kila kijiji.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja amefika baadhi ya vijiji na kusaidia ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kutumia fedha za mfuko wa jimbo.

Habari Kubwa