Mgogoro ardhi wananchi na mwekezaji waibuka

25Nov 2018
Beatrice Shayo
Kibaha
Nipashe Jumapili
Mgogoro ardhi wananchi na mwekezaji waibuka

MGOGORO wa eneo lenye zaidi ya ekari 560 Kibaha mkoani Pwani, umeibuka huku wananchi wakilalamikia njama za viongozi wa wilaya kutaka kuwafukuza kwa madai kwamba linamilikiwa na mwekezaji.

waziri wa ardhi william lukuvi picha na mtandao

Hatua hiyo imebainika baada ya zaidi ya wakazi 600 wa kijiji cha Madabala, Kata ya Mbwawa wilayani humo, kulalamikia viongozi wa serikali kwa madai ya kutaka kuwapora ardhi hiyo na kuitoa kwa mwekezaji.

Wananchi hao walililamikia mgogoro huo wa ardhi ambao unaendelea baina yao na mwekezaji huyo, Hashim Saggaf, ambaye wanadai kuwa viongozi wa wilaya ya Kibaha wanamlinda.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, Mwenyekiti wa Wakulima Wakazi wa Madabala, Ali Abdallah, alisema tangu mwaka 1990 walianza kuishi katika eneo hilo lakini wanashangazwa na kauli za viongozi wa wilaya kudai wamevamia.

Alisema mwaka 2010 ulitokea mgogoro baina ya mwekezaji huyo na kesi kufikishwa katika Baraza la Ardhi la Kata na baadaye Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.

Abdallah alisema kesi hiyo ilidumu miaka mitano na hukumu ilitolewa mwaka 2015 kuwa wananchi hao wana haki baada ya mlalamikaji kukosa kujitokeza mahakamani.

Alisema mwaka 2018 walijitokeza viongozi wa wilaya na kuwajulisha kuwa eneo hilo ni la mwekezaji, jambo ambalo liliwashtua wakati hukumu ilishatolewa mahakamani.

"Tulimwomba atupatie nyaraka zinazoonyesha kuwa yeye ni mmiliki wa eneo hili lenye ekari 561 lakini hatukuonyeshwa. Hapa tunafanyiwa ubabe, askari wanakuja kutusumbua. Tulifika hadi wizarani kuangalia hilo shamba linaloitwa namba 443 tukajulishwa kuwa halipo," alisema.

"Tunamwomba Rais (John) Magufuli afahamu kuwa tatizo la rushwa halijaisha Kibaha. Viongozi wanawatuma watu kutuvunjia maeneo yetu ambayo tulishinda kesi Mahakama Kuu, leo hii wanataka hili eneo tumwachie huyu wanayesema ni mwekezaji," alisema.

Pia alisema walishaandika barua kwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, kuhusiana na mgogoro huo ili achukue hatua na kabla ya kupatiwa majibu, viongozi wa wilaya wameanza kuwasumbua huku wakimlinda mwekezaji.

Naye Antony Masilamba alisema wanamwomba Rais Magufuli pamoja na Waziri Lukuvi kuingilia kati mgogoro huo ili wapate haki yao kama mahakama ilivyofanya.

"Kabla hatujapata majibu kutoka kwa Waziri tumeanza kusumbuliwa na viongozi wa Wilaya ya Kibaha na wote wako upande wa mwekezaji, yaani sisi wananchi hatuna mtetezi wala hatuna haki," alisema.

VIONGOZI WAJITETEA

Kutokana na mgogoro huo, mwanzoni mwa wiki hii, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Theresia Mmbando, aliwatuma maafisa wa mipango miji mkoa kwenda kwenye shamba la hilo ili kusikiliza malalamiko ya wananchi pamoja na viongozi wa serikali wa eneo husika kabla ya kufanya uamuzi.

Hata hivyo, Ofisa Mipango Miji katika Sekretarieti ya Mkoa wa Pwani, Speratus Ruteganya, alisema mgogoro huo umeshaenda mahakamani na kwamba mahakama ndicho chombo huru cha kutoa haki na uamuzi utakaotolewa unaheshimiwa na pande zote.

Ruteganya alisema eneo hilo ni sehemu ya mamlaka ya serikali za mitaa na liko chini ya Halmashauri ya Mji Kibaha, hivyo haiwezekani mtu kumilikishwa shamba kubwa namna hiyo.

Mtendaji wa Kata hiyo, Francis Shayo, alidai kuwa wananchi wanaolalamika ni wavamizi na shamba hilo ni mali ya Hashim Saggaf, ambaye alilinunua kwa wananchi wa Mbwawa mwaka 1986.

Hata hivyo, alipotakiwa kutoa uthibitisho wa vielelezo vya umiliki wa shamba hilo kama wanavyo ofisini kwao wakiwa viongozi wenye dhamana ya kujua umiliki wa ardhi katika maeneo yao, alishindwa kufanya hivyo na kudai kuwa alisikia tu kwa viongozi waliopita.

Mtoto wa Saggaf, Abdallah Saggaf, alipofuatwa na waandishi wa habari kuzungumzia mgogoro huo, aligoma kufanya hivyo.