Mgombea urais NRA ataka mdahalo na Lissu

20Oct 2020
Thobias Mwanakatwe
Nipashe
Mgombea urais NRA ataka mdahalo na Lissu

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha NRA, Leopold Mahona, ameomba mdahalo kati yake na mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ili aweze kupimana naye ubavu katika kujenga hoja zenye mashiko.

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha NRA, Leopold Mahona.

Ametoa ombi hilo jana wakati  akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili kuhusu changamoto alizozibaini katika siku 53 hadi sasa tangu kuanza kwa kampeni za uchaguzi mkuu zilizoanza Agosti 26, mwaka huu.

 

"Naomba kama kuna 'media' ambayo inaweza kuandaa mdahalo na Tundu Lissu ili nione je, hizo pointi anazosema anaweza kuzitetea vizuri au ni maneno ya jukwaani tu, maana kuna maneno ya jukwaani na maneno ya utendaji," alisema.

 

Mahona alisema inasikitisha hadi uchaguzi unakaribia kumalizika hakuna hata chombo chochote cha habari ambacho kimejitokeza kutaka kuandaa mdahalo kati yake na Lissu.

 

Alisema tatizo kuna kasumba kwa media hapa nchini kung' ang'ania kutaka kufanya midahalo na wagombea wa vyama vinavyojipambanua kuwa ni vikubwa kitu ambacho kimsingi siyo cha kidemokrasia kwa sababu vyama vyote viko sawa.

 

"Kwa muda mrefu nimekuwa nataka nifanye mdahalo na Lissu lakini nimekuwa natafuta fursa siipati," alisema.

 

Mahona alisema katika kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka huu, vipo baadhi ya vyombo vya habari yakiwamo magazeti na televisheni ambavyo haviandiki wala kutangaza habari za baadhi ya wagombea jambo ambalo linatia ukakasi katika demokrasia nchini.

 

Aliongeza kuwa kama taifa moja tunatakiwa kuwa kitu kimoja kwa kutengeneza mazingira ambayo yataleta ushindani wa huru na wa haki.

"Tunataka uwanja wa demokrasia katika siasa uwe sawa sawa, haiwezekani mgombea mmoja anapewa zaidi kipaumbele kwenye vyombo vya habari wakati Sheria ya Gharama za Uchaguzi ipo wazi," alisema.

Septemba mwaka huu, mgombea urais kupitia CHADEMA, Lissu, alikuwa akisisitiza kwenye mikutano yake ya kampeni akitaka afanye mdahalo na mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Rais John Magufuli.

Habari Kubwa