Mgombea aahidi wanawake SACCOS

22Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
SERENGETI
Nipashe
Mgombea aahidi wanawake SACCOS

MGOMBEA wa ubunge wa Jimbo la Serengeti mkoani Mara, Catherine Ruge (CHADEMA), amejinadi kwa wanawake na kuahidi kuwa endapo akichaguliwa kuwa mwakilishi wa wananchi wa jimbo hilo, ataanzisha SACCOS maalum kwa ajili yao ili kuwawezesha kupata mikopo.

MGOMBEA wa ubunge wa Jimbo la Serengeti mkoani Mara, Catherine Ruge (CHADEMA).

Akizungumza kwenye mkutano wa ndani uliowajumuisha baadhi ya wanawake Jimbo la Serengeti bila kujali itakadi zao za vyama, Ruge aliwaomba kumchagua na kuwa mbunge wao ili ahakikishe anawaletea maendeleo ikiwamo kuunda SACCOS kwa lengo la kukopa kwa riba nafuu.

"Niwaombe wanawake wenzangu mnipigie kampeni kwa wapigakura ili nikichaguliwa kuwa mbunge nitatue matatizo yenu kwa sababu nayajua ikiwamo ukosefu wa mitaji, lakini mkinichagua nitaenda kuwatetea bungeni pamoja na kuanzisha SACCOS kwa lengo la kukopa na kulipa kwa riba ya gharama nafuu,"  alisema Ruge.

Alisema, Jimbo la Serengeti linakabiliwa na changamoto ya majisafi na salama jambo ambalo akiingia bungeni atalipigania na kuhakikisha kuwa wanawake wanapata huduma hiyo.

Mgombea huyo aliongeza kuwa sababu kubwa inayomsukuma kuanzisha SACCOS, ni kutaka kuwasaidia wanawake ambalo ni kundi linalobeba familia.

Kwa upande wake, Magreth Juma, alimwomba mgombea huyo kuwatetea na kuhakikisha anatimiza ahadi na asije akawageuka.

Magreth aliongeza kuwa wanawake na wananchi wa Serengeti kwa ujumla wanahitaji kupata uwanja wa ndege ili kuongeza mapato kutokana na watalii kuingia na kutoka mbuga ya Serengeti.

Weisiko Genya, alisema kuwa umeme wanaotumia wilayani hapo unasumbua endapo mbunge huyo atafanikiwa kuchaguliwa awasaidie kutatua tatizo hilo.

Habari Kubwa