Mgombea ataka aweke historia urais

28Sep 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Mgombea ataka aweke historia urais

MGOMBEA urais wa kupitia Chama cha Alliance for Democratic Party (ADC), Queen Sendiga, amewaomba Watanzania kumchagua ili awe rais wa kwanza mwanamke na kuingia katika historia, huku akiahidi kufanya mageuzi makubwa katika sekta mbalimbali nchini.

Alisema akipata nafasi hiyo atahakikisha anatengeneza mazingira wezeshi ya ajira kwa Watanzania ikiwa ni pamoja na kuimarisha sekta binafsi nchini.

Akizungumza jana katika moja ya mkutano wake wa kampeni jijini Dar es Salaam, alisema ili kuwa na uchaguzi wenye amani ni vyema Watanzania wakatunza tunu hiyo.

Aliahidi kuwa endapo atachaguliwa kushika nafasi hiyo, anajiamini kuleta mageuzi makubwa nchini katika sekta zote zinazogusa maisha ya wananchi.

“Ninajiamini, uwezo nilionao ni mkubwa, Watanzania waniamini, nitasimamia kwa kiwango kikubwa kuweka mifumo bora na imara ya kuliletea maendeleo taifa letu, naomba mnipigie kura,” alisema Sendiga.

Kwa mujibu wa mgombea huyo, vipaumbele vyake vitakuwa ni pamoja na kulinda haki za wanawake, watoto na makundi maalum, pia tatizo la ajira kwa vijana.

Sendika ni miongoni mwa wanawake wawili kati ya wagombea 16 kwa upande wa Tanzania Bara ambao wamejitosa katika kinnyang’anyiro cha urais.

Licha ya ukata unaovikabili vyama vingi vya upinzani katika kufanya kampeni, mgombea huyo ameonekana maeneo mbalimbali nchini akinadi sera za chama chake kwa wapigakura.

Mgombea mwingine mwanamke katika nafasi hiyo ni Cecilia Mwanga, kupitia Chama cha Demokrasia Makini.

Habari Kubwa