Mgombea NCCR kuunganishailani za vyama

14Sep 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Mgombea NCCR kuunganishailani za vyama

MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia Chama cha NCCR-Mageuzi, Yeremia Maganja, amesema akiingia madarakani ataunganisha ilani za uchaguzi za vyama vyote kupata moja kwa ajili ya kuendesha serikali miaka mitano ijayo.

Akizungumza na Nipashe kuhusu namna chama hicho kilivyojiandaa kwenye kampeni na kitakavyoingia madarakani, Maganja alisema lengo la kuunganisha ni kupata ilani bora ambayo itawaunganisha wote kulingana na matamanio yao.

Alisema katika kuchambua ilani hizo, watatumia wataalamu wabobezi (think tank) katika sekta zote nchini ambao hawafungamani na chama chochote cha siasa ili kuhakikisha kwamba inapatikana moja ambayo ni bora zaidi.

“Sisi tunaamini kwamba kila ilani ya uchaguzi ya kila chama cha siasa ina baadhi ya mambo ambayo ni mazuri, tukiingia madarakani tutakusanya ilani zote na kuzipeleka kwa wataalamu watuchambulie yale mazuri na kupata moja ambayo ndiyo itatumika kuendesha serikali kwa miaka mitano,” alisisitiza Maganja.

“Na kwa sababu tumepanga kwamba tukiingia madarakani tutatengeneza Katiba mpya, hilo ni miongoni mwa mambo ambayo tutaliingiza ili chama chochote kinachoingia madarakani kifuate utaratibu huo, na ilani hizo zitakuwa zinakusanywa miezi minne kabla ya uchaguzi na kuchambuliwa na wataalam ili anayekuwa anaingia madarakani aitumie hiyo.”

Kwa mujibu wa Maganja, atahakikisha wanapitia upya mchakato uliotumika kuwaondoa wafanyakazi wote kazini kwa madai ya vyeti feki.

Alisema kwamba kama hawakulipwa jasho lao baada ya kufukuzwa, serikali yake itahakikisha inawalipa wote.

“Hawa wafanyakazi walioondolewa kazini, waliajiriwa kihalali na serikali, kwa hiyo kama ni makosa serikali ndiyo ilifanya. Kwa hiyo tukiingia madarakani, tutaanza upya ‘ku-review’ (kupitia) namna walivyoingia, walivyofanya kazi na namna serikali ilivyotekeleza kazi ya kuwaondoa,” alisema Maganja.

“Tunaamini kwamba hata kama walifoji vyeti, lakini serikali iliwaamini na ndiyo iliyowaajiri na wamelitumikia taifa wengine miaka 10, 20, 30, kwa hiyo huwezi kuwaondoa kienyeji hivi, lazima tutaliangalia hili kwa upya na tutalifanyia kazi, na kama kuna haki zao ambazo walistahili kulipwa na hawakufanyiwa hivyo, sisi tutalifanya kwa kushauriwa wa wataalamu ikiwamo Shirika la Kazi Duniani (ILO).”

“Tutaangalia waliingiaje, makosa yao na ya serikali katika kuwaingiza kazini yalikuwa yapi, hawa ni binadamu kwa hiyo lazima tuangalie namna pia walivyotoka ili kuifanya sekta ya umma iwe ya kuheshimika.”

Mgombea huyo alisema endapo wataingia madarakani ni watahakikisha kwamba wanafunzi wote waliopata ujauzito na kufukuzwa shule wanarejea masomoni.

“Wanafunzi hawa wataendelea na masomo mpaka pale ambapo wataalamu wa afya watathibitisha kwamba wanahitaji kusimama kwa ajili ya kujifungua na baada ya hapo watarejea shuleni kuendelea na masomo kama kawaida,” alisema Maganja.

“Mwanaume na mwanamke wanatakiwa kupewa fursa sawa, tunaamini kwamba suala la wanafunzi kupata ujauzito kunasababishwa na mambo mengi ikiwamo mazingira tuliyonayo ambayo si rafiki pamoja na matatizo mengine, kwa hiyo ili haki itendeke kwa watoto wote wa kike na kiume kupata elimu, hatutamfukuza shule.”

Alisema kuendelea kufukuza wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito shuleni ni kuendelea kutengeneza taifa tegemezi.

Habari Kubwa