Mgombea udiwani Chadema aahidi kuanzisha Saccos ya kata

16Sep 2020
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Mgombea udiwani Chadema aahidi kuanzisha Saccos ya kata

Mgombea udiwani wa Kata ya Ngokolo Manispaa ya Shinyanga kupitia CHADEMA, Emmanuel Ntobi, amenadi sera zake kwa wananchi wa kata hiyo, na kutoa ahadi ya kuboresha Elimu, Afya, kujenga Soko, Kituo cha Polisi, barabara, pamoja na kuanzisha Saccos kwa kila kata kuinua wananchi kiuchumi.

Mgombea udiwani Kata ya Ngokolo manispaa ya Shinyanga (CHADEMA), Emmanuel Ntobi, akinadi sera zake kwa wananchi wa Kata hiyo ili wamchague kuwa diwani wao kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Ntobi alitoa ahadi hizo jana Septemba 15,2020 wakati akizundua rasmi kampeni zake kwenye Kata ya Ngokolo, mkutano uliofanyika kwenye Kiwanja cha Ngokolo Mitumbani, na kuhudhuliwa pia na Mgombea ubunge wa Jimbo la Shinyanga mjini kupitia Chadema Salome Makamba.

Alisema ndani ya miaka mitano katika utawala wake alipokuwa diwani wa kata hiyo, kuna vitu vingi ambavyo amevifanya kwa ajili ya maendeleo ya wananchi, na kuomba wampe tena mitano mingine ili akamilishe miradi mingine ambayo alikuwa ameianza pamoja na kuinua wananchi kuichumi kwa kuanzisha Saccos ya kata.

“Kwenye uongozi wangu nilipokuwa diwani kuna vitu vingi ambavyo nimevifanya, ujenzi wa Ghuba, kukarabati shule mbili za msingi Mwadui na Mapinduzi, kujenga Kituo cha Polisi Mtaa wa Majengo kipo kwenye hatua za mwisho, ujenzi wa barabara kiwango cha lami, na utatuzi wa migogoro,” alisema Ntobi.

 

 

 

 

 

“Pia nilitafuta wafadhili kutoka Denmark walinipatia vifaa tiba, vikagawiwa kwenye maeneo mbalimbali ya huduma za afya hapa manispaa, ambapo vifaa hivyo vilitumwa lakini mpaka sasa vimezuiliwa bandarini bila ya sababu za msingi,” aliongeza.

Aidha alitaja vipaumbele vyake endepo wananchi wakimchagua tena kuwa diwani wao, atajenga kituo cha afya, kumalizia kituo cha Polisi, kuboresha sekta ya elimu , kujenga Soko, Garden ya kupumzikia wananchi , pamoja na kuanzisha Saccos ya kata ambayo itasaidia kuinua uchumi wa wananchi.

Katika hatua nyingine alitaja sababu za kufukuzwa mara kwa mara kwenye vikao vya baraza la madiwani la Manispaa ya Shinyanga, kuwa inatokana na kupigania masuala ya ufisadi ikiwamo kupinga ungezeko la Tozo kwenye vibanda vinavyomilikiwa na manispaa, nakubainisha hata Rais John Magufuli alilisema alipokuwa Shinyanga.

Alisema kitu kingine ni kupinga kupandishwa wananchi bei ya kuuziwa viwanja na Manispaa ya Shinyanga, kutoka Shilingi 500,000 hadi Milioni 2, na kudai aliundiwa njama za kutolewa nje ya kikao ili bajeti hiyo ipitishwe.

Kwa upande wake mgombea ubunge wa jimbo la Shinyanga mjini Salome Makamba kupitia chama hicho, amewataka wananchi wa Kata hiyo wasifanye makosa siku ya Oktoba 28, bali wampigie kura Emmanuel Ntobi ili awe diwani pamoja na yeye, na Mgombea urais Tundu Lissu ili wakafanye kazi pamoja ya kuwaletea maendeleo.

Habari Kubwa