Mgombea urais Aahidi kufuata nyayo za Shein

29Sep 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Mgombea urais Aahidi kufuata nyayo za Shein

MGOMBEA urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha ADA- TADEA, Juma Ali Khatib, amesema akichaguliwa kuwa rais wa Zanzibar anakusudia kufuata nyayo za rais Dk. Ali Mohamed Shein kwa kuendeleza na kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati, ambayo lengo lake kubwa ni kukuza uchumi na kuongeza ajira ..

kwa vijana.

Khatib alisema hayo wakati akizindua kampeni za chama chake katika uwanja wa Magaeni Sogea, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Alisema miradi yote muhimu iliyobaki, ambayo imesimamiwa na Rais Shein anakusudia kuimaliza, ili kuunga mkono kazi nzuri iliyofanywa katika kipindi cha miaka kumi ya uongozi wake.

“Nikichaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar, nakusudia kutekeleza miradi yote muhimu ya kimkakati ikiwamo ujenzi wa bandari ya Mpigaduri iliyopo Maruhubi, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja...nitajenga uwanja wa ndege wa Karume uliopo Pemba, ili kuruhusu kutua ndege kubwa na kuongeza idadi ya watalii,” alisema.

Khatib ambaye ni waziri asiye na wizara maalumu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, alimshukuru Rais Dk. Shein kwa kumjumuisha katika Baraza la Mawaziri na hivyo kupata uzoefu wa hali ya juu wa uongozi.

“Namshukuru Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kuniteua kuingia katika Baraza la Mawaziri na hivyo kupata uzoefu mkubwa wa uongozi,” alisema.

Alisema akichaguliwa kuwa rais, anakusudia kufufua eneo la viwanda vidogo liliopo Amani kwa ajili ya kuzalisha ajira nyingi za vijana na kurudisha enzi ya Zanzibar ya kupiga hatua kubwa katika sekta hiyo.

Pia, alisema katika miaka ya 1980, Zanzibar ilikuwa maarufu kwa kuwa na viwanda vingi vidogo vya aina mbalimbali ikiwamo masufuria, sabuni, nyaya za umeme pamoja na mafuta ya nazi na kusafirisha nje ya nchi.

“Mimi nilibahatika kufanya kazi katika Shirika la viwanda vidogo viliopo Amani...tulikuwa tukizalisha bidhaa mbalimbali na kusafirisha nje ya nchi,” alisema.

Naye mgombea mwenza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya ADA - TADEA, Hassan Kijogoo, alisema wanakusudia kuifanya Zanzibar kuwa lango kuu la uchumi kwa kusafirisha bidhaa mbalimbali hadi katika visiwa vya Ngazija.

“Tukichaguliwa kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano chini ya mgombea John Shibuda, tunakusudia kuifanya Zanzibar kuwa lango kuu la kiuchumi kwa kutumia fursa zilizopo za nchi jirani ikiwamo Ngazija na Mombasa Kenya,” alisema.

Habari Kubwa