Mgombea urais atinga NEC akiwa pekupeku

08Aug 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Mgombea urais atinga NEC akiwa pekupeku

MGOMBEA wa urais kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Mutamwega Mgaiwa, jana alifika kwenye Ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kugombea nafasi hiyo akiwa hajavaa viatu (pekupeku).

Mgaiwa alitinga katika ofisi hizo akiwa amefuatana na Mgombea Mwenza wake, Satia Musa Bebwa na viongozi wachache wa chama hicho, ambao kabla ya kuingia ukumbi wa kuchukulia fomu, walipofika walipiga magoti na kusujudu na kudai kuwa wao ni watoto wa mkulima na hawalimi wakiwa wamevaa viatu.

Akizungumza baada ya kuchukua fomu, mgombea huyo alisema kuna Watanzania wengi hadi leo hawana viatu, hivyo wao wapo pamoja na wanyonge.

“Vipaumbele vyetu ni amani, upendo na umoja na tunataka kumkomboa mkulima apate bei nzuri ya pamba kwa kilo Sh. 5,000 kulingana na soko la dunia, kahawa Sh. 5,000, korosho Sh. 5,000 ndiyo lengo letu kumkomboa mkulima.

“Tumesujudu hii ardhi kuashiria kwamba amani itatawala na kila kitu kwenye dunia ni ardhi, ardhi ndio mama wa kila kitu na Tanzania yetu tunataka ibaki na ardhi yetu kama kawaida,” alisema mgombea huyo ambaye amewahi kuwa Mbunge wa Mwibara mkoani Mara.

Mgombea Mwenza, Satia, alisema lengo lao ni kumnyanyua mkulima na kilimo kisonge mbele, akifafanua: “Tunamtaka Mrisho Mpoto kwa kuwa amekuwa akitetea wanyonge na tunataka kuungana naye."

MGOMBEA ADC

Naye Mgombea wa Chama cha Alliance for Democratic Change(ADC), Queen Sendiga 'Mama wa Taifa', alichukua fomu akiwa ameambatana na mgombea mwenza Shoka Khamis Juma, huku wakiahidi watahakikisha huduma za afya na elimu zinatolewa bure.

MGOMBEA UPDP

Mgombea wa nane aliyechukua fomu jana ni wa Chama cha United People's Democratic Party (UPDP), Twalib Kadege, akiwa ameambatana na mgombea mwenza wake, Ramadhani Ali Abdallah, alisema watakwenda kutafuta wadhamini kwa matakwa ya tume.

“Kaulimbiu yetu UPDP safi na umoja daima, na tunaamini umoja utawezesha kupata kiti cha urais, tumejipanga kwa hilo, tukimaliza taratibu za kusaka wadhamini, ndiyo tutasema vipaumbele vyetu, na utafutaji wa wadhamini tutaanzia Dodoma na tunaamini wagombea wetu watachaguliwa na tutapata wabunge wengi,” alisema Kadege.

Habari Kubwa