Mgombea urais NCCR kufuta sheria kandamizi

26Oct 2020
Na Mwandishi Wetu
MARA
Nipashe
Mgombea urais NCCR kufuta sheria kandamizi

MGOMBEA urais kupitia NCCR-Mageuzi, Jeremiah Maganja, ameahidi kubadilisha sheria kandamizi kwa jamii endapo atashinda uchaguzi huu na kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

MGOMBEA urais kupitia NCCR-Mageuzi, Jeremiah Maganja.

Alitoa ahadi hiyo jana katika mkutano wa kampeni Jimbo la Tarime Mjini mkoani Mara wakati akiomba kura.

Alisema akipatiwa ridhaa na wapigakura ataenda kubadilisha sheria zinazoonekana kuwa kandamizi kwa ustawi wa wananchi, huku akiboresha uchumi wa taifa na kutengeneza mazingira rafiki kwa mfanyabiashara.

Mganja aliongeza kuwa atahakikisha anaimarisha Muungano wa Tanzania na Zanzibar, na kuondoa kero ndogo ndogo zinazokwamisha kufikia maendeleo ndani ya muungano huo.

“Mimi mkinipa ridhaa ya kuwa Rais nitasimamia mchakato wa katiba mpya ya Jaji Joseph Sinde Waryoba ambayo itashirikisha wananchi kutoa maoni, ili kukamilika na kutumika, nitasimamia kuboresha elimu na miundombinu yake ili wanafunzi wakapate elimu bora,” alisema na kuendelea:

“Pia nitaenda kufuta michango iliyo kero kwa wazazi na walezi, na wanafunzi watasoma bure msingi hadi chuo, nitahakikisha walimu wanaenda semina za mara kwa mara kukabiliana na mitaala ya kisayansi kadiri inavyokuja, nitahakikisha ninaboresha uchumi wa Taifa hili ili kila mfanyabiashara na Mtanzania kunufaika na rasilimali zilizopo.”

Kuhusu afya,  Maganja alisema kuwa atafuta vitambulisho vya bima ya afya kwa sababu amegundua kuwa wengi walio na kadi ya vitambulisho hivyo hawanufaiki na matibabu, badala yake wanaambiwa kwenda kununua dawa madukani, huku bima hizo zikibagua baadhi ya magonjwa ya kutibu.

Naye mgombea ubunge wa NCCR Mageuzi Jimbo la Tarime Mjini, Mery Nyagabona, alisema kuwa akipewa ridhaa ya kuwa mbunge atajenga hoja ya kujenga soko ambalo limebomolewa ili wafanyabiashara waende kufanya biashara upya na kukuza mitaji na uchumi wa halmashauri.

Habari Kubwa