Mgombea urais Zanzibar asimamishwa ACT

21Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
Dar
Nipashe Jumapili
Mgombea urais Zanzibar asimamishwa ACT

MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT - Wazalendo), Khamis Idd Lila, ambaye juzi alipewa ulinzi binafsi na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), amesimamishwa uanachama na chama chake.

Mgombea urais kwa tiketi ya ACT - Wazalendo, Khamis Idd Lila katikati.

Chama hicho kimemsimamisha uanachama mgombea huyo katika kikao chake cha Kamati Maalum kilichokaa Zanzibar juzi, baada ya kupokea taarifa rasmi kuwa aliyekuwa mgombea wao wa urais kwa kushirikiana na Ali Makame Issa, wamepinga msimamo wa chama hicho.

Taarifa iliyotolewa na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Juma Said Sanani, ilisema wanachama hao kwa makusudi waliamua kupingana na msimamo wa chama kwa maslahi yao binafsi.

Alisema watu hao wamekidhalilisha na kukiingiza chama kwenye mgogoro usiokuwa na sababu kwa kuandika barua ya kushiriki uchaguzi wa marudio ambao chama kilishapeleka barua kwa Zec tangu Februari 9, ya kutoshiriki uchaguzi huo.

“Kwa kitendo chao hicho... Kamati maalum imewasimamisha rasmi uanachama kwa mujibu wa Katiba ya ACT Ibara ya 11 (2) kuanzia leo kwa ukiukwaji mkubwa wa katiba Ibara ya 7(3)(5)(9), ibara ya 10 (2)(c)(d),Ibara ya 22(1)(2)(4),” alisema Sanani.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya ACT Wazalendo, masuala yote ya kinadhamu kwa viongozi na wanachama yanashughulikiwa na Kamati za maadili za ngazi husika na kwa kuwa kwa sasa Kamati hizo hazijaundwa, Kamati ya Uongozi ya Taifa ndiyo inayoshughulika na mambo yote ya nidhamu.

“Hivyo jambo hili linawasilishwa mbele ya Kamati ya Uongozi ya Taifa kwa hatua zaidi na kwa taarifa zaidi naambatanisha na tamko la Chama katika kikao cha tarehe 13 Februari,2016 kilichofanyika Dar es Salaam.

Juzi wagombea saba wa nafasi ya urais wa Zanzibar walikabidhiwa rasmi walinzi kutoka Jeshi la Polisi Zanzibar, akiwemo Lila.

Wengine waliokabidhiwa walinzi ni Juma Ali Khatib (TADEA), Soud Said Soud (AFP), Hamad Rashid Mohamed(ADC), Issa Mohamed Zonga(SAU), Hafidh Hassan Suleiman (TLP), na Ali Khatib Ali (CCK).

Mgombea wa CCK Ali huenda akawa katika hatari kama ya Lila kwani naye chama chake kilishatangaza kutoshiriki katika uchaguzi huo wa marudio.

Alipozungumza na Nipashe jana, Mwenyekiti wa CCK, Constantine Akitanda, alisema hana taarifa za mgombea wao kupewa ulinzi kwasababu walishaweka msimamo wa kutoshiriki uchaguzi huo.

Habari Kubwa