Mgomo wa daladala watikisa Dodoma

14Jan 2021
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Mgomo wa daladala watikisa Dodoma

MADEREVA daladala jijini Dodoma, jana waligoma kutoa huduma ya usafiri kwa abiria kwa saa kadhaa, wakishinikiza kufanyiwa ukarabati eneo la stendi ya Sabasaba.

Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya madereva walidai eneo hilo halijafanyiwa ukarabati licha ya kulilalamikia kwa muda mrefu, huku wakiendelea kulipa ushuru kila siku.

Mmoja wa madereva hao, Ayoub Mazengo, alisema licha ya wao kulipa ushuru kila siku kwa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, miundombinu ya stendi hiyo ni mibovu.

Alisema pamoja na kutofanyiwa ukarabati, kero nyingine ni eneo hilo kuwa dogo, kushindwa kukidhi idadi ya daladala.

“Tumekuwa tukitoa ushuru kila siku, lakini hakuna kinachofanyika na hivi sasa msimu wa mvua eneo linakuwa shida kupitika kutokana na tope na mashimo yanayotokana na mvua, lakini eneo hili ni dogo na kuna wafanyabiasahra wengine wanalitumia,” alisema Mazengo.  

Alisema pamoja na eneo hilo kutokuwa na miundombinu rafiki pia kitendo cha wafanyabiashara wengine wa mboga na matunda kulitumia imekuwa usumbufu kwao.

“Pamoja na wafanyabiashara hawa wa mboga na matunda, wako watu ambao wanafanya biashara ya kuchoma mahindi na mishkaki wanaotumia majiko ya moto ambayo ni hatari kwa magari kwani yanaweza kulipuka moto na kuleta maafa,” alisema.

Soma zaidi: https://epaper.ippmedia.com

Habari Kubwa