Mgonjwa mpya corona abainika Zanzibar

26Mar 2020
Rahma Suleiman
Zanzibar
Nipashe
Mgonjwa mpya corona abainika Zanzibar

MGONJWA wa pili wa corona ametambuliwa Zanzibar ambaye ni raia wa Ujerumani mwenye umri wa miaka 27.

Waziri wa Afya Zanzibar, Hamad Rashid Muhammed, picha mtandao

Raia huyo ni mke wa raia wa Ghana, ambaye aligundulika kuwa na virusi vya corona wiki iliyopita, ambaye anaendelea na matibabu katika kituo maalum kilichotengwa na serikali kilichopo Kidimni.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa Afya, Hamad Rashid Muhammed, alisema kuwa wiki moja iliyopita mtu huyo alipimwa na akagundulika kuwa hana corona na kuwekwa karantini.

Waziri Hamad Rashid alisema kuwa jana alipopimwa aligundulika kuwa na ugonjwa huo.

“Huyu mama tulikuwa tukifuatilia taarifa zake, na jana alipimwa tena na kugundulika kuwa na virusi hivyo, ambavyo ameambukizwa na mumewe,” alisema Hamad.

Alisema serikali inaendelea kuwapatia huduma ili wasiwaambukize wengine.

Aidha, waziri huyo alisema pia kuna mtu mmoja kisiwani Pemba ambaye anashukiwa kuwa na corona na amewekwa katika karantini ili kuendelea kufanyiwa uchunguzi.

Waziri Hamadi alisema watu 65 wamewekwa karantini kwa siku 14 ili kuendelea kufanyiwa uchunguzi.

Alieleza kuwa anasikitishwa na baadhi ya watu waliowekwa katika karantini kitoheshimu taratibu zilizowekwa.

Alisema baadhi wamekuwa wakigoma kula chakula kwa madai kuwa gharama zake ni kubwa.

Alieleza kuwa serikali imefunga milango yake haitaki raia yeyote kutoka nje ya Zanzibar kwa lengo la kudhibiti ugonjwa huo usiendelee kuenea.

Hata hivyo, alisema kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekua wakiuza bidhaa za kujikinga na corona ambavyo vimeshapita muda wake wa matumizi.

Alisema kuwa serikali imelifungia duka moja la dawa kwa kuuza dawa ya kunawia mikono ambayo ipo chini ya kiwango.

Habari Kubwa