Mhadhiri kuburuzwa kortini kwa madai rushwa ya ngono

14Aug 2020
Renatha Msungu
Dodoma
Nipashe
Mhadhiri kuburuzwa kortini kwa madai rushwa ya ngono

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Ofisi ya Mashtaka, inatarajia kumfikisha mahakamani Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Jacob Nyangusi (43), kwa tuhuma za kutaka rushwa ya ngono.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa jana, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Dodoma, Sosthenes Kibwengo, alisema mtuhumiwa huyo alikutwa na TAKUKURU majira ya saa 3:00 Oktoba 3, 2018 nyumbani kwake, eneo la Nyumba 300.

Alisema TAKUKURU ilimkamata mtuhumiwa huyo kabla hajatenda nia ovu ya kufanya ngono na mwanafunzi wake wa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Sanaa katika Jiografia na Mazingira.

"Tumemfungulia shauri Nyangusi kwa tuhuma za kutaka rushwa ya ngono kinyume cha kifungu cha 25 cha Sheria ya Kupambana na Rushwa namba 11/2007," alisema Kibwengo.

Kibwengo alisema awali, TAKUKURU ilipokea taarifa kwamba mtuhumiwa alimtaka mwanafunzi wake kingono ili kumsaidia mitihani ya marudio na kumwezesha kufaulu na ndipo ikaweka mtego na kumkamata.

Kibwengo alisema kwa kushirikiana na Ofisi ya Mashtaka imewafikisha mahakamani Theobald Maina (44) aliyekuwa Diwani wa Kata ya Ntyuka jijini hapa, Benedict Mazengo (60) ambaye ni ofisa mtendaji na Anderson Jonathan aliyekuwa Mwenyekiti wa Mtaa wa Chimala.

Wote hao, alisema wanashtakiwa kwa makosa ya matumizi mabaya ya mamlaka kinyume cha kifungu cha 31 na ubadhirifu kinyume na kifungu cha 28 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007.

Kibwengo alisema uchunguzi umeonyesha kwamba Aprili, 2016 watuhumiwa kwa pamoja walitumia vibaya madaraka yao, hivyo kujipatia kwa njia ya kughushi Sh. Milioni mbili ambazo ni malipo ya minara ya simu iliyoko kwenye Kata ya Ntyuka.

Alisema watuhumiwa walifuja fedha hizo badala ya kusimamia ili zitumike kwa ajili ya kununua vifaa vya ujenzi wa ofisi ya mtaa wa Ntyuka.

Pia alisema TAKUKURU itamfikisha katika mahakamani ya Hakimu Mkazi Dodoma, Ritha Mapunda (30), ambaye alikuwa Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mnadani jijini Dodoma na kwa tuhuma za kuomba rushwa ya Sh.400,000 kinyume cha kifungu cha 15 (a) cha Sheria Na. 11/2007 ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa.

Habari Kubwa