Mhagama ataka vijana kujiunga kwenye vikundi

21Apr 2016
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Mhagama ataka vijana kujiunga kwenye vikundi

WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye ulemavu, Jenister Mhagama, amekemea tabia ya kulaumu serikali na kuwataka vijana wajiunge katika vikundi vya ujasiriamali ili wapewe mafunzo na mikopo ya kuendeleza kazi zao.

Jenister Mhagama.

Alisema hayo baada ya kukagua na kuzindua Kikundi cha vijana mafundi seremala cha (KIMASEMO), kilichopo kata ya Sabasaba Manispaa ya Morogoro.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano ni ya kufanya kazi, sio kushinda baa ama kucheza ‘pool’. Alisema Tanzania ya sasa inaelekea kwenye kujitegemea na kuachana na wafadhili ambao wamekuwa wakitoa misaada kwa masharti na manyanyaso.

Aidha, aliiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro kuwapa eneo la kudumu vijana hao la kutengeneza na kuonyesha bidhaa zao ili waweze kupata soko.

“Biashara ni matangazo, naiagiza halmashauri kutenga eneo ili hawa vijana waonyeshe biashara zao, ili mradi wasiharibu mazingira na pia kulipa kodi,” alisema.

Alimuagiza mkuu wa wilaya ya Morogoro, kuwapatia vijana hao mafunzo ili wajue namna ya kutengeneza samani zitakazouzwa ndani na nje ya nchi.

Alisema kupitia bajeti ya mwaka wa fedha 2016/2017, atatenga fungu kwa ajili ya kuwapa mafunzo vijana hao na kuwawezesha waweze kukuza mitaji yao na kupata fursa ya kukopa kwenye taasisi za fedha.

Hata hivyo, aliwataka wadau kuunga mkono kazi wanazofanya vijana hao kwa kununua bidhaa wanazotengeneza na kuwataka vijana wengine kujiunga katika vikundi ili awaweze kusaidiwa.

Mbunge wa Jimbo la Morogoro Mjini Abdul Aziz Abood, alikisaidia kikundi hicho kwa kutoa hundi ya Shilingi milioni mbili na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, aliahidi kukisaidia kikundi hicho Sh. milioni 10 kwa ajili ya kununua vitendea kazi.