Mhandisi Kasekenya awapongeza TANROADS Arusha

18Apr 2021
Na Mwandishi Wetu
Arusha
Nipashe Jumapili
Mhandisi Kasekenya awapongeza TANROADS Arusha

​​​​​​​SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoani Arusha, imekamilisha miradi ya kitaifa ya ujenzi wa barabara za Sakina hadi Tengeru (njia nne) zenye Kilometa 14.1, barabara ya mchepuko wa Kusini (Arusha Bypass) yenye Kilometa 42.4 pamoja na ujenzi wa barabara ya Kia hadi-

-Mererani Kilometa 26 ambazo zote zimejengwa kwa kiwango cha lami na kukamilika kwa asilimia 100.

Akiongea na watumishi hao wa TANROADS, mara baada ya kumaliza ziara ya kukagua barabara hizo Naibu, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amewapongeza watumishi hao kwa kusimamia vyema miradi ya ujenzi wa barabara hizo na kuhakikisha inakamilika kwa viwango vilivyoainishwa kwenye mikataba ya ujenzi wake.

“Nataka niwahakikishie kuwa, Serikali ya awamu ya sita kupitia Rais wetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, itaendelea kusimamia utekelezaji wa miradi yote ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara iliyopo, lakini pia miradi mipya itakayotengewa fedha kwenye bajeti ya Serikali katika mwaka wa fedha wa 2021/2022, nayo itatekelezwa” Amesema Kasekenya.

Naibu Waziri Kasekenya amekuwa katika ziara ya siku moja mkoani Arusha akitokea Dodoma kupitia barabara ya vumbi ya Kongwa kwenda Kibaya hadi Arusha (kilometa 430), ambapo kwa sasa usanifu wa barabara hiyo umekamilika na ujenzi wake utatangazwa mara baada ya kutengewa fedha katika bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2021/2022.

Habari Kubwa