Mhandisi matatani mabomba ya bil. 3/-

27Jan 2019
Cynthia Mwilolezi
Arusha
Nipashe Jumapili
Mhandisi matatani mabomba ya bil. 3/-

NAIBU Waziri wa Wizara ya Maji, Jumaa Aweso, ameagiza kutafutwa popote alipo aliyekuwa Mhandisi wa Maji Wilaya ya Karatu na kurudishwa kujibu tuhuma za kuweka mabomba mabovu ya thamani ya Sh. bilioni tatu kwenye mradi wa vijiji 10.

Mkandarasi wa kampuni ya Meru Constructions, Ayo Jeremia (wa pili kulia) na Mhandisi wa Maji wa wilaya ya Monduli, Charles Saidea, wakiwa chini ya ulinzi baada ya kushikiliwa kwa amri ya Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Juma Aweso baada ya kubaini kuwapo kwa udanganyifu katika mradi wa Maji unaoendelea katika kijiji cha Lendenyika wilayani Monduli juzi. PICHA: MPIGAPICHA WETU

 

Aweso alitoa agizo hilo jana wilayani humo wakati wa ziara yake ya siku moja na kuahidi kurejea wilayani baada ya shughuli za bunge kuisha wiki mbili zijazo, ili aweze kuonana na Mhandisi huyo aliyehamishiwa sehemu nyingine na waliohusika wengine waliofanya uhuni huo.

 

Alisema haiwezekani serikali itoe fedha zote hizo ili wananchi wapate maji lakini maji hayapo na watu wamehamishiwa maeneo mengine wanaendelea kula raha huku wananchi wakiteseka.

 

"Siwezi kuruhusu mhandisi anayeharibu Karatu kuhamishiwa sehemu nyingine. Huyu ni kumng'oa tu maana ataharibu na kwingine," alisema.

 

Naibu Waziri alisema hawezi kutembelea maeneo ya vijiji vya mradi mpaka wiki mbili zijazo ili akutane na mhandisi aliyekuwepo wakati huo ampe majibu sahihi uso kwa uso.

 

Aidha, aliagiza watendaji wa wizara yake kushughulikia nyaraka za madai ya Sh. milioni 45 zilizopelekwa Mei 23, mwaka jana, ili mkandarasi kampuni ya Engineering Plus (T) Limited anayetekeleza mradi wa maji kwa Tom alipwe kwa ajili ya kukamilisha mradi.

 

Baadhi ya vijiji vilivyoko kwenye mradi huo ni  Endamagha, Kusumay, Endanyaweti, Matala, Mikocheni, Lugeli na Kasisay.

 

Aweso alisema hakuna mbadala wa maji kama ilivyo kwenye vyakula vingine, hivyo mradi huo lazima ukamilike na kwamba atakayehujumu hataonewa huruma.

 

Naye  Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo, alimwomba Naibu Waziri Aweso kuwapigania ili kutatua changamoto za maji walizo nazo wilayani humo.

 

Alisema mradi wa vijiji 10  ulikamilika mwaka 2013, lakini maji hayapatikani kwa wananchi sababu ya mabomba yaliotumika kupasuka kabla ya wananchi kutumia maji hayo wakati waliofanya kitendo hicho wakiwapo.

 

Mahongo alisema mahitaji ya maji katika mji wa Karatu ni mita za ujazo 4,700,  lakini zinazopatikana kwa sasa ni  720 ambazo hazitoshi kulinganisha na mahitaji halisi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Karatu, Jubleti Mnyenye, alimwomba Naibu Waziri kutembelea mradi wa maji katila vijiji 10 ambao tangu umalizike mwaka 2012 maji hayatoki.

 

Pia aliomba wasaidiwe kuyafikisha maji bonde Eyasi ambalo linatumika kuzalisha vitunguu na kusafirishwa nchini Kenya, lakini changamoto maji ya kumwagilia hayatoshi.

 

Mbunge wa Karatu, Willy Qambalo, alimwomba Aweso kutembelea baadhi ya vijiji vya miradi ili ajionee watu walivyokula fedha bila kukamilisha kazi waliyopewa na bado wahusika waliofanya hivyo hawajachukuliwa hatua.

 

 

 

Habari Kubwa