MIAKA MIWILI KIFO CHA FARU FAUSTA:

27Nov 2021
Sanula Athanas
DAR ES SALAAM
Nipashe
MIAKA MIWILI KIFO CHA FARU FAUSTA:
  • Kazi kubwa imefanyika kudhibiti ujangili

NI vigumu kuuzungumzia uchumi wa Tanzania pasi na kuutaja utalii. Sekta hiyo sasa inachangia robo ya fedha za kigeni na asilimia 17.5 ya Pato la Taifa.

Faru Fausta.

Kadri unavyozama kuuchambua utalii huo, unakutana na makundi makuu ya wanyamapori ambao ndiyo vivutio vinavyosafirisha wageni kutoka mbali kuja nchini kuwashuhudia.

Hapo unabaini kuna wanyama wakubwa watano ambao ni tembo, faru, twiga, nyati na simba.

Unapodokeza mnyama faru, hapo ndipo shida inaposikika. Kwa nini? Wanyama hao  ambao wamekuwa kivutio kikuu cha watalii, katika miaka ya karibuni walitajwa kuwa katika hatari ya kutoweka kiasi cha kutikisa mwelekeo wa taifa.

Wakati kuna mtazamo wa jumla, katika mustakabali wa kipekee, leo hii ni siku maalum kwa wadau wote wa wanyamapori na washirika wa sekta ya utalii, kwa maana ya kumbukumbu ya MIAKA MIWILI kamili tangu kifo cha Faru Fausta.

Huyu ni aliyekuwa faru mzee zaidi si tu kwa Tanzania, bali pia dunia nzima, akishikilia rekodi hiyo. 

Ni faru aliyekuwa na upekee wake kuanzia jina la 'ubatizo' Faru Fausta, aliyeaminika ndiye mzee zaidi duniani.

Faru Fausta alikufa tarehe kama ya leo mwaka juzi kwenye Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro akiwa na umri wa miaka 57.

Kabla ya kifo chake, Faru huyo jike alikuwa chini ya uangalizi maalum kwa kipindi cha miaka mitatu kutokana na afya yake kudhoofika na kuanza kushambuliwa na wanyama wakali mwituni.

"Faru Fausta kwa mara kwanza alionekana katika eneo la Ngorongoro mnamo mwaka 1965 na mwanasayansi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), akiwa na umri wa kati ya miaka mitatu na minne.

"Ilipofika mwaka 2016, afya yake ilianza kudhoofika. Wanyama wakali, hususani fisi, walianza kumshambulia na akapata vidonda vikubwa sana. Ilibidi tumtoe porini na kumweka kwenye uangalizi maalum.

"Vidonda vyake vilipona lakini afya yake bado ilikuwa dhoofu, hivyo hatukumrejesha porini," alisimulia Dk. Freddy Manongi, Mhifadhi Mkuu wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, katika taarifa ya kifo chake miaka miwili iinayotimu leo.

Mnyama huyo alishika hadhi ya kitaifa, kwa kuwa mwaka 2017 suala la matunzo yake lilifikia hatua ya kuibua mjadala kisiasa ndani ya Bunge, mada kuu katika hoja zote zilibeba mtazamo wa msimamo wa maslahi yake.

Ofisa Mwandamizi wa Uhifadhi wa Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Philbert Ngoti, anasema udhalimu wa ujangili  uliwakumba wanyamapori hao, hata kutikisa ustawi wao.

Takwimu za Shirika la Uhifadhi Duniani (IUCN), zinabainisha kuwa katika miaka ya 1970 Tanzania ilikadiriwa kuwa na faru 10,000 huku Hifadhi ya Taifa Serengeti pekee ikiwa na wanyama hao wapatao 700.

Tayari shirika hilo limeshatangaza kuwa wanyama aina ya faru weusi ambao wako 750 katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ni miongoni mwa viumbe vilivyo hatarini kutoweka duniani.

Vilevile, Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF), linabainisha kuwa Tanzania imepoteza takriban asilimia 99 ya faru weusi katika kipindi cha miaka 40 iliyopita.

Sababu ni nini? Ngoti ambaye pia Mratibu wa Faru nchini, anawanyoshea kidole majangili kuwa ni sehemu ya mzizi wa tatizo lililobadili historia ya nchi na hata kuelekea kuwa hasi zaidi.

Anasema Tanzania ni nchi iliyotamba duniani kwa idadi kubwa ya faru, lakini kutokana na baa la ujangili, iligeuka kuwa na hifadhi ya kubahatisha ya wanyama hao, tukio la kiharamia lilizozikabili pia nchi nyingi duniani.

Kutokana na hali hiyo, Ngoti anasema serikali ilichukua hatua mbili kuu, ikiwa ni pamoja na ukali uliopitiliza katika ulinzi wa wanyamapori, ambao sasa askari wake wanaowajibika ni jeshi kamili.

Anasema serikali pia iliumiza kichwa kwa njia ya pili inayotokana na faru waliopelekwa ughaibuni Afrika Kusini wakawe mahali salama na rahisi kuzaliana, wakiwa katika hesabu ya wanandugu tisa waliorejeshwa katika hifadhi za nyumbani Novemba 10 mwaka juzi.

Ofisa huyo anabainisha kuwa kuchukuliwa kwa hatua hiyo ya nchi kupeana faru, ni sehemu ya utekelezaji wa Mkataba wa Kimataifa wa Kusimamia Viumbe Vilivyo Hatarini Kutoweka (CITES).

Ngoti anasema kuwa katika maisha hayo mapya, faru hao waliotoka ughaibuni na ndugu zao wa nyumbani, jumla yao ilifika 190 kwa takwimu zilizoishia Machi mwaka jana, huku lengo kuu la nchi ni wafike 205 kufikia mwaka 2023, yaani miaka miwili ijayo.

Mtaalamu huyo wa wanyamapori, anafafanua mchakato wa kuzaliana kwamba mimba ya faru inachukua kati ya miezi 15 na 16. Kwa lugha rahisi, ni wastani wa mwaka mmoja na robo.

Anasema mikakati iliyochukua imesaidia kuongeza idadi ya wanyama hao nchini, akiweka wazi kuwa mwaka 2018, nchi ilikuwa na faru 161 na hadi kufikia Machi mwaka jana, walifikia 190, likiwa ni ongezeko la faru 29 ndani ya miaka miwili.

"Hadi Machi mwaka huu, kulikuwa na faru 190 katika Hifadhi ya Taifa Mkomazi na Great Serengeti Ecosystem," Ngoti anabainisha.

Ofisa huyo anaanisha ukanda huo wa ikolojia ya Serengeti unajumuisha Hifadhi ya Taifa  Serengeti, Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro, mapori ya Ikorongo, Maswa na Hifadhi ya Taifa ya Masai Mara iliyoko Kenya.

Ngoti anasema mpango uliopo ni kuwatawanya ndugu wa Faru Fausta katika makazi mapya ndani ya hifadhi za taifa: Burigi-Chato na Arusha.

Anabainisha faru sasa wanalindwa kwa kifaa maalum cha kufuatilia mienendo yao na taarifa zao kupokewa kwenye vituo mbalimbali kwa teknolojia ya kisasa.

“Pembe za wanyama hawa huuzwa China na Vietnam ambako hutengeneza dawa za kienyeji ambazo huaminiwa zinatibu homa, kupooza, saratani na kuongeza nguvu za kiume.

"Kwa Vietnam mtu kuwa na jambia au kifaa kilichotengenezwa kwa pembe ya ndovu ni ufahari mkubwa ndiyo maana watu wa huko hutoa fedha nyingi ili kupata kiungo hicho.

“Kwa sasa ujangili umepungua, kulikuwa na vigogo wa ndani ya serikali walishirikiana na watu wa nje kuangamiza wanyama hawa.

"Mkakati uliopo sasa ni kusafisha ndani na ndiyo maana tumeleta jeshi la uhifadhi na misitu," Ngoti anafafanua.

Hakika, tunapoadhimisha miaka miwili ya kofi cha Faru Fausta, tuna kila sababu ya kuipongeza serikali kupitia mamlaka zake za uhifadhi, kwa jitihada kubwa zilizofanyika kuwanusuru wanyamapori dhidi ya ujangili!

Habari Kubwa