Miaka 100 auawa na fisi

12Apr 2017
Stephen Chidiye
TUNDURU
Nipashe
Miaka 100 auawa na fisi

KIKONGWE anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 100, Asyenepe Laia, amefariki dunia baada ya kuvamiwa na kushambuliwa na fisi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, baada ya fisi hao kumuua, katika tukio lililotokea Alhamisi iliyopita, waliondoka na mwili wake kwenda katika msitu ulioko jirani na eneo analoishi na kula nyama yake.

Mashuhuda hao walisema katika tukio hilo, Asyenepe alikamatwa na fisi hao alipokuwa anaokota kuni ajili ya kuchochea  katika moto alio kuwa ameuwasha ndani ya nyumba yake.

Walisema tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Kalulu Mashambani kandokando na Hifadhi ya Msitu Hifadhi ya Taifa ya Selous katika Tarafa ya Matemanga, Tunduru mkoani Ruvuma.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Tunduru, Dk. Gaufrid Mvile, alisema chanzo cha kifo hicho kilisababishwa na kitendo cha wanyama hao kumshambulia.

Alisema katika tukio hilo walikuta mabaki ya vipande viwili vya mifupa, michirizi ya damu na mabaki ya nguo, mambo yaliyoashiria kuwa kikongwe huyo aliuawa na fisi hao na kumla nyama yake yote.

Naye Ofisa Wanyamapori wa Wilaya ya Tunduru, Limbega Ally, alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kwamba tayari amekwishatuma askari wenye silaha kwa ajili ya kuwasaka fisi hao na kuwaua ili wasiendelee kuleta madhara kwa watu wengine.

Habari Kubwa