Miaka 60 ilivyotia fora

10Dec 2021
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Miaka 60 ilivyotia fora

RAIS Samia Suluhu Hassan kwa mara ya kwanza ameongoza sherehe ya maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara zilizotia fora kwenye Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam jana.

Rais Samia Suluhu Hassan, akipunga mkono kwa wananchi wakati akiwasili kwa gari maalum la Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (JWTZ), katika Uwanja wa Uhuru, mkoani Dar es Salaam jana, kwa ajili ya sherehe za maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara. picha: ikulu

Sherehe hiyo ya maadhimisho ya siku ya uhuru wa nchi ilihudhuriwa na marais kutoka nchi jirani na maelfu ya Watanzania, ikiwa ni ya kwanza kwa Rais Samia tangu aapishwe kushika nafasi hiyo Machi 19 mwaka huu baada ya kifo cha Dk. John Magufuli Machi 17 mwaka huu.

Baada ya kuwasili uwanjani huko, Rais Samia alikagua gwaride maalumu lililoandaliwa kwa ajili ya siku hiyo muhimu.

Marais waliohudhuria sherehe hizo ni: Uhuru Kenyatta wa Kenya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Paul Kagame wa Rwanda, Filipe Nyusi wa Msumbiji, Othman Ghazali wa Visiwa vya Comoro ambaye pia ni Makamu Mwenyeti wa Pili wa Umoja wa Afrika (AU).

Viongozi wengine waliokuwapo kwenye Uwanja wa Uhuru jana ni Rais mstaafu wa Malawi Joyce Banda na Rais mstaafu wa Msumbiji, Joackim Chissano.

Wengine ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Jean-Michel Lukonde na Makamu wa Rais wa Burundi, Prosper Bazombanza.

Pia kulikuwa na wajumbe maalumu waliowawakilisha marais na wakuu wa nchi za Botswana, Uganda, Afrika Kusini, Zimbabwe, Oman na Eswatin.

Mbali na wageni hao, sherehe hiyo pia ilihudhuriwa na marais wastaafu wa Tanzania, mabalozi, wabunge na wawakilishi wa jumuiya za wafanyabiashara.

Kwenye sherehe hizo zilikuwapo burudani mbalimbali ikiwamo ngoma za asili kutoka makabila na maeneo tofauti nchini, wasanii na halaiki ya wanafunzi wa shule za msingi.

Rais Samia aliwashukuru wageni na wananchi wote waliohudhuria sherehe hiyo.

ILIVYOTIA FORA

Katika sherehe hiyo wananchi na viongozi waliohudhuria walipata fursa kuona shughuli mbalimbali za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kivutio kikubwa kilikuwa ni halaiki ya wanafunzi zaidi ya 600 waliotengeneza maumbo yenye ujumbe tofauti.

Pia gwaride la vikosi vya ulinzi na usalama vilitia fora huku Jeshi la Uhamiaji likishiriki kwa mara ya kwanza baada ya kuanzishwa kwake kisheria miezi miwili iliyopita.

Baada ya viongozi waalikwa kuwasili uwanjani hapo, Rais Samia akiwa kwenye gari maalumu la jeshi, aliingia na kuzunguka uwanja kusalimia maelfu ya wananchi waliojitokeza.

Wimbo wa Taifa na Wimbo wa Afrika Mashariki ziliimbwa kisha mizinga 21 kupigwa na baadaye alikwenda kukagua gwaride rasmi lililoandaliwa kuadhimisha miaka 60 ya uhuru.

Baadaye kulikuwa na maonesho maalumu la makomandoo wa JWTZ walioshuka kwenye chopa kwa kamba kisha watoto wa halaiki wakahitimisha burudani kwa kuchora maumbo mbalimbali yaliyoonekana kuwavutia waliohudhuria.

Katika hatua nyingine, jana jioni Rais Samia aliwatunuku nishani maalumu ya miaka 60 ya uhuru Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji.

*Imeandikwa na Romana Mallya na Christina Mwakangale.

Habari Kubwa