Mibuyu hifadhini yadaiwa kuwa maficho ya majangili

17Jan 2017
Jaliwason Jasson
BABATI
Nipashe
Mibuyu hifadhini yadaiwa kuwa maficho ya majangili

MITI ya mibuyu katika Hifadhi ya Tarangire inadaiwa kutumiwa na majangili kujificha ili kukwepa mapambano ya kukabiliana na vitendo hivyo.

Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na mkuu wa kitengo cha utalii katika hifadhi hiyo, Benard Mgina, wakati akizungumza na Nipashe.

“Ndani ya hifadhi hii miti ya mibuyu ni mingi sana ambayo inatumiwa mara nyingine na wanyama kama tembo kama chakula chao kwani wanapoitafuna wanakuta ina maji mengi ambayo huwasaidia kukabiliana na kiu.’’

"Watalii kutoka nchi za Ulaya wanakuja na kuona miti iliyoharibiwa na tembo ikiwa na mapango makubwa wanashangaa na kuona ni kama maajabu kwao, lakini majangili nao wanatusumbua sana, wanatumia miti hiyo iliyochimbwa na tembo kujificha ndani ili tusiwaone askari wetu wanapofanya doria," alisema Mgina.

Alisema majangili hao wanaitumia miti hiyo kama mapango ya kujificha na kuwafanya askari wao kupata wakati mgumu kukabiliana na ujangili ingawa wameshagundua mtandao wao na kuutokomeza.

"Miti hiyo pamoja na kutumiwa sana na tembo kama chakula, lakini pia inatumiwa na ndege zaidi ya aina 500 waliomo kwenye hifadhi hiyo kwa ajili ya makazi hali inayowavutia watalii," alisema.

Alisema hifadhi hiyo inakadiriwa kuwa na tembo 3,000 ambao ni kivutio kikubwa kwa wageni wanaotoka maeneo mbalimbali ya Ulaya na Asia wanafika kila mwaka.

Hata hivyo, Mgina alisema licha ya vivutio vilivyopo ndani ya hifadhi hiyo, idadi ya watalii wa ndani ni ndogo sana hivyo amewaomba kuitembelea kwa wingi ili wajionee uzuri na maajabu yaliyomo.

Habari Kubwa