Michango ujenzi vyoo yazua jambo bungeni

12Jun 2019
Sanula Athanas
DODOMA
Nipashe
Michango ujenzi vyoo yazua jambo bungeni

 MBUNGE wa Nkasi, Ally Keissy (CCM), ameliomba Bunge kurejesha fedha zilizochangwa na wabunge kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya mfano kila jimbo nchini kwa kwa madai kwamba mradi huo umekwama.

 MBUNGE wa Nkasi, Ally Keissy (CCM).

Baada ya kumalizika kwa kipindi cha 'Maswali' bungeni jijini Dodoma jana, mbunge huyo alisimama na kutumia Kanuni ya 47 ya Kanuni za Kudumu za Bunge, akitaka chombo hicho cha kutunga sheria kiahirishe shughuli zake za jana na kujadili hoja hiyo ya dharura.

Katika kujenga hoja yake, Keissy alihoji  kwa nini hakuna mrejesho uliotolewa kwa wabunge kuhusu fedha walizochanga wakishirikiana na wadau wengine kufanikisha ujenzi wa vyoo bora kwenye majimbo yote nchini.

Alisema inasikitisha kuona tangu jambo hilo lianze kutekelezwa kwa kukusanya fedha kwa wabunge na wadau wengine wa maendeleo hadi jana hakuna mrejesho uliotolewa bungeni maendeleo ya ujenzi huo.

Keissy aibainisha kuwa hata majimboni vyoo hivyo bado havijajengwa, hivyo kulitaka Bunge kurejesha fedha kwa wabunge na wadau wengine waliochanga kama suala hilo limeshindikana.

"Mheshimiwa Naibu Spika, ni muda mrefu zaidi ya mwaka  tangu tuanze kutoa michango kwa ajili ya kupata pesa za ujenzi wa vyoo bora vya mfano katika majimbo  yetu, hatujapewa mrejesho hili suala limefikia wapi, wala kiasi kulichokusanywa, nimekuwa nikiuliza, ila sipewi majibu, sasa basi kama imeshindikana turudishiwe pesa zetu tutajenga wenyewe," Keissy alisema.

Baada ya mbunge huyo kutoa hoja, wabunge wengi walisimama kumuunga mkono, lakini Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, alisema hoja hiyo haikuwa ya dharura, hivyo hakukuwa na uhalali wa kujadiliwa na Bunge kulingana na masharti ya Kanuni za 47 na 48 za Kanuni za Kununi za Bunge.

Hata hivyo, Dk. Tulia alisema suala hilo linasimamiwa na Spika na "liko mikono salama na hata fedha zilizochangwa ziko salama" na wakati utakapofika wabunge watapewa taarifa.

Alisema fedha zilizotolewa na wadau nazo ziko salama huku akiwataka wale ambao bado hawajakamilisha ahadi zao, wafanye hivyo ili kuhakikisha wanapata fedha na kujenga vyoo bora vya mfano.

Juni 22, mwaka jana, Bunge lilizindua kampeni ya ujenzi wa vyoo vya mfano shuleni, huku Spika Job Ndugai akibainisha kuwa hali ya vyoo katika shule nyingi nchini ni mbaya.

Uzinduzi huo ulifanyika kwenye Viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, akiwa mgeni rasmi.

Katika hafla ya uzinduzi huo, Spika Ndugai alisema wabunge wote walikuwa wameshachangia Sh. milioni 81 huku wabunge wa majimbo wakichanga Sh. milioni 528 (kila jimbo Sh. milioni mbili kwa majimbo yote nchini).

Alisema hali ya vyoo katika shule nyingi zinazomilikiwa na serikalini ni mbaya na inahatarisha maisha ya wanafunzi.

Spika Ndugai alibainisha kuwa kuna ongezeko kubwa la wanafunzi katika shule nyingi za umma nchini kutokana na uamuzi wa serikali ya awamu ya tano wa kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari.

Ndugai alisema idadi ya wanafunzi imeongezeka lakini miundombinu ya kujifunzia na kufundishia vikiwamo vyoo bado haijaongezwa na kuboreshwa.

Alisema ni kutokana na changamoto hiyo, Bunge limeamua kuanzisha kampeni hiyo ya kukusanya fedha kwa ajili ya kujenga vyoo vya mfano katika kila jimbo nchini ili wadau wengine watakaojitokeza wavijenge kunusuru afya za wanafunzi.

Alisema zipo shule ambazo vina vyoo hatarishi kwa afya za watumiaji na kwamba katika shule nyingi vyoo vilivyopo havikidhi mahitaji ya watu wenye ulemavu na watoto wa kike.

Alisema vyoo vya mfano vitajengwa kwa kuzingatia makundi matatu ya watu wenye mahitaji maalum, watoto wa kike na vya watoto wa kiume.

"Fedha tulizopata ni za kuanzia na tunaendelea kuchangia kwa kadri tutakavyoelekezwa na kamati yetu," alisema.

Kiongozi huyo wa Bunge alisema jumla ya Sh. bilioni 3.5 zinahitajika kwa ajili ya kujenga vyoo vya mfano katika majimbo yote 264 nchini.

Katika uzinduzi wa kampeni hiyo siku hiyo, jumla ya Sh. bilioni 1.45 zilikusanywa kutoka kwa wadau mbalimbali zikiwamo wizara, wabunge, taasisi za umma na kampuni wa watu binafsi.

Habari Kubwa